Thursday, September 30, 2010

Kama huku kunawezekana basi na kwingine inawezekana, ama huku si Tanzania?

school_feeding  Watoto wakipata msosi shuleni.

Katika shule za msingi Nkweseko (1937), Nkwawangya (1975) na Nkwamwasi (1962) zilizoko Machame wilayani Hai chakula cha mchana hutolewa shuleni. Nimeelezwa kuwa mahudhurio ya watoto ni kati ya 97%-98% na kiasi kinachobaki cha wasiohudhuria kinatokana na sababu za ugonjwa.

 

Wamewezaje kufikia hilo? Ni sera ya wilaya nzima ya Hai, nimeambiwa…labda na wilaya nyingine pia mkoani Kilimanjaro hufanya hivo sijui…wazazi huchangia sh 8,000 kwa kila mwaka ambazo hutumika kulipa posho ya mlinzi na mpishi, kununua kuni na mafuta. Pia mzazi huchangia debe 1 na nusu la mahindi na kilo 5 za maharage kwa mwaka. Mboga za majani watoto hujilimia wenyewe shuleni.

 

Ukisoma taarifa za wizara ya elimu na utamaduni utaona kuwa utoro na hasa mahudhurio ya shule katika sehemu nyingi Tanzania unasababishwa na kutokuwa na chakula cha mchana mashuleni kwani watoto wengine wanaishi mbali na shule na umaskini. Hivyo hawarejei shuleni na ni shida kwa watoto wadogo zaidi wa shule za awali na walio na ulemavu.

 

Sasa, kama ndo hali hii, wilaya fulani inakuwa na sera fulani nzuri ama inafuata maelekezo yaliyoko kwenye sera kwa nini isiwe kila mahali ama sera ya elimu inatekelezwa kwa viraka viraka? Au watunga/watekelezaji sera wa Hai wana uelewa mbovu ama mzuri kuliko wa sehemu nyingine Tanzania?

Safari ni ndefu lakini safari moja huwa inaanzisha nyingine…

Tuesday, September 28, 2010

Usilalamike kwa kuwa pengine Brain-drain ilianza zamani kuliko unavyofikiria!

Mlango Chagga Hse Mlango ukiwa na tundu la usalama

 

Ukiangalia mlango wa asili wa kichaga na makabila mengine utaona kuna tundu/tobo ambalo tunaelezwa ni kwa ajili ya ulinzi (kuangalia nani yuko bomani kama kuna hodi ama kusikika kwa sauti isiyokuwa ya kawaida bomani). Ukienda katika hoteli kubwa kokote utakuta kuna katobo mlangoni ambako aliyeko nje haoni ndani ila wa ndani anamuona aliyeko nje mlangoni kwa kuwa kana kioo kimkuzacho aliye nje.

 

Wachaga na Wakikuyu wanasali kuangalia kaskazini uliko mlima Kilimanjaro na Kirinyaga (Kenya). Waislamu husali kunako kibra ambayo lazima iwe kaskazini!

 

Wachaga na makabila mengine wawaliokuwa wanatoka mlimani (ama wanaishi huko ama kwenda kutambika/kusali) walipokuwa wanashuka wakikutana na watu wanaelekea uelekeo wa mlima (uphill) aliyepaswa kusalimu mwingine ni yule atokaye mlimani kwa kuwa alikuwa na ‘utakatifu fulani’ baada ya kukutana na Mungu ana kwa ana. Utakatifu huu wazeza usiwe kama wa Mt. Simon Kitururu…lol! Ukiangalia sheria za usalama barabarani za kiingereza ambazo tunazitumia sisi hapa nchini utaona kuwa mwenye gari apandishaye mlima hupewa fursa ya kupita na ashukaye mlima kwa heshima zote, ama?

 

Mila na desturi ni tamu wajameni….! Lakini ndo hivo tena twaibiwa na wajanja tuliowafungulia mlango kisha tukang’oa bawaba na mlango ukabaki wazi ili manyang’au wa kila aina waingie kunyumba!!!

Taswira toka mgombani!

Chagga hse 1

Wadau wakishangaa nyumba ya jadi ya kichagga!

Chagga hse11

Nyumba ya kichagga!

Chach-Julie kili

Hapo vipi? Pozi la mlima Kilimanjaro linapamba taswira!

Monday, September 27, 2010

Nipe sababu za msingi kwa nini nichange!

arusi

Kwa kawaida arusi zimekuwa zikitumia fedha nyingi.

 

Nimeelezwa na rafiki yangu kuwa arusi ya ndugu yake iligharimu shilingi za kitanzania milioni 60. Kasema pia kuwa kuna ambazo amehudhuria zimegharimu zaidi ya shilingi milioni 200.

 

Nimesikia kuwa kitakwimu, mwaka jana katika Tanzania gharama za arusi zilifikia dola za kimarekani bilioni moja…sina hakika ila kama hali ndo hii ninayoiona naweza kuamini.

 

Ninashangaa inapoitishwa michango ya elimu na afya hakuna anayejitokeza kwa hiyo naomba unipe sababu za msingi zitakazonishawishi nikuchangie katika arusi yako, ya mwanao ama ya ndugu yako.

Saturday, September 25, 2010

Tatizo ni nini?

Mitindo ya kulala 

Aina za kulala!

Kaka Ngw’anambiti, pole na majukumu! Mimi ni msomaji wako katika kijiji chako ambacho sijui nani alikuchagua kuwa mwenyekiti wake! Nimekuandikia kutaka mchango wako wa mawazo. Unaweza kubandika hapo kwenye ubaraza wako ili wengine wajifunze kupitia suala linalonikabili. Naitwa mama John (si jina halisi) na niko Dar.

 

Mimi ni mama wa watoto watatu. Mimi na mume wangu tulioana wakati tukiwa wabichi kabisa kutoka chuoni na sasa tunakaribia miaka 12 tangu tuoane. Siku za hivi karibuni nimekumbwa na tatizo moja. Niligundua kuwa mume wangu hana hamu nami kabisa na tunapopata nafasi ya kujamiiana huwa anapiga ‘bao moja tu’ na kuchoka kitu ambacho si kawaida yake. Nilimuuliza lakini hakutaka kuwa muwazi kwangu japo alisingizia kuwa ni kuchoka tu na mihangaiko ya mchana.

 

Majuzi tulipata mgeni nyumbani kwetu…mdogo wangu wa kike asomaye chuo kikuu kimoja hapa nchini. Ilikuwa akae nasi mpaka watakapofungua chuo mwezi wa 11 baada ya kunyimwa fursa ya kuwa chuoni mwezi wa 10 kama ratiba inavyoonyesha katika prospectus zao.

 

Alipofika, baada ya muda akanilalamikia kuwa shemejie anamtaka kimapenzi na hivyo anataka kuondoka hapo nyumbani aende kijijini kwani hataki kuleta usumbufu katika familia yangu. Baada ya kufikiri tulikaa na kuzungumza na mdogo wangu na tukaamua kuwa ni lazima tufanye kitu ili kuzuia ubaradhuli wa namna hii usirejee tena kwake na kwa wengine.

 

Tulikubaliana kuwa mdogo wangu amkubalie na wapange kukutana usiku baada ya mimi kulala. Kwa kuwa muda mwingi huwa anarejea nyumbani usiku na kwa kuwa chumba cha wageni alalacho mdogo wangu kiko karibu na sebule atamgongea dirishani kasha atamfungulia. Tulikubaliana kuwa siku ya siku mimi ndie nitalala kwenye chumba hicho nay eye atakwenda kulala chumba cha watoto na kazi ya kufungua mlango nitaifanya mimi.

 

Alimweleza kuwa ‘ombi lake limekubaliwa’ na wakapanga kuwa wataonana jioni na kuwa agonge dirisha. Baada ya kula jioni mdogo wangu alikwenda kulala chumba cha watoto na mimi nikazima taa ya sebuleni kasha kulala chumba cha wageni. Mume wangu alikuja akagonga dirisha na nikaenda kumfungulia mlango. Kwa sababu ya giza hakuweza kunitambua na akavua viatu ‘visipige kelele vikaniamsha’ nakujitoma chumba cha wageni kimyakimya. Alinivamia na kuanza shughuli.

 

Naomba niseme kuwa alipiga bao 4 non-stop huku akinisifia (akidhani kuwa ni mdogo wangu) kuwa nayajua majambo. Kisha akatoa wallet (gizani) na kuipa pesa laki moja!!! Kabla hajaondoka nilimwambia nikimnong’oneza kuwa angoje nikamfungulie. Nilikwenda nikawasha taa na alipatwa na mshangao na mshtuko kuniona ni mimi!!!!

 

Nilimwambia, ‘baba John, kumbe ndivyo ulivyo?’ Sikuendelea ila kulia kwa uchungu na aliniomba msamaha kwa kitendo kile kwani nilimweleza A-Z kuhusu jinsi alivyofanya.

 

Najiuliza, kwa nini mimi nilikuwa napewa nusu dose na kwa ‘mdogo’ wangu ikapatikana full dose? Je wanaume wote mko hivyo? Naomba msaada wa mawazo…nifanyeje? Je hatanitenda tena?

Haya wadau, naomba msaada wenu wa mawazo…Kaka Kaluse na Kamala uwanja ni wenyu kwani hili nadhani ni suala la kiutambuzi pia japo linajumuisha saikolojia pia!

Thursday, September 23, 2010

Ninatamani mila hii irudi…lol!

 

shikome

Kitu namna hii hapo zamani ilikuwa bomba sana!

 

Juzi tulikaa na wazee wa kichaga panapo moto usiku…kwa wasukuma wanaita moto huo shikome ama luganga na hata kwetu tunaita ekekome ambapo wazee na watoto wanakutana na kusimuliwa hadithi za zamani zenye mafundisho mbalimbali. Ni kwa namna hiy o ambapo pamoja na kutoa mafunzo juu ya maisha lakini pia kunakuwa na mapokeo ya mila, desturi, maonyo, na elimu kwa watoto (Intergenerational knowledge transfer) toka kwa wakubwa.

 

Shikome/luganga yaweza kutengenezwa kwa kuni ama kinyesi cha ng’ombe ama mbuzi (muyanga kwa kisukuma) na wakati mnaongea viazi vilitumbukizwa ndani ya huo moto, vingine vililiwa hapo na vingine vilitumbukizwa humo na kuachwa kwa ajili ya kula asubuhi (kwa wanafunzi na waendao shamba) vikisokomezewa na togwa ama maziwa (kwa wakurya) na maziwa kwa wasukuma! Maisha yalikuwa poa sana!

 

Sasa ulimwengu wa utandawazi-wizi umetufanya wazee (samahani, baada ya kukaa na wazee kwa siku chache nami najiona bonge la kikongwe…lol!) tusiwe na nafasi na watoto na watoto wamekengeuka…wameota mapembe…wazee na watoto hawataki vumbi wanataka kiyoyozi (full kipupwe) kama wanavosema wenyewe. Wanataka kula chips kuku/mayai (chips za kukaangwa kwa mafuta ya transformer na mayai/kuku wa kufugwa kwa kulishwa antibiotics!).

 

Hawataki kula michembe, matobholwa (viazi), hawataki togwa wanataka thoda na chai!!!! Hawataki kula dona wanataka sembe! Hawataki kula mtama/ulezi ati utaonekana weye wa hali ya chini (kwa mujibu wa baadhi ya koo za kisukuma huko Bariadi na Maswa!!).

 

Kaazi kweli kweli! Natamani mila hizi zirudi, lakini kivipi? Nani ataanza?

Taswira!

Chachkili

Uso si muhimu bali mlima Kilimanjaro unaoonekana kwa mbali!

Nyerere tree 1961

Nyerere Tree: Inasemekana mti huu ulipandwa na Mwalimu Nyerere mwaka 1962 na bado upo hapo shule ya msingi Nkwamwasi, Machame.

Trad Chagga food

Baadhi ya vyakula vya asili vya kichagga! Nadhani mnavifahamu au sio?

Tuesday, September 21, 2010

Precisionair na Biashara za Kilimbukeni

photo

Kwa muda sasa tumekuwa na shirika moja la ndege ambalo kwa bahati nzuri ni la kibinafsi. Hata hivyo tofauti na matarajio ya wengi wetu kuwa kwa kuwa shirika la ndege la taifa (Air Tanzania) linalegalega lingeweza kuleta huduma bora kwa watanzania na kuwafanya wasaha machungu ya shirika lao la kitaifa ‘kunyongwa’ hadi likafa kutokana na sera mbovu.



Jumatatu ya tarehe 20 September 2010 mgeni wangu alikuwa anasafiri toka Kilimanjaro kwenda Dar na ndege nambari PW 0433 (walipoingia ndegeni wakaelezwa kuwa ni ndege nambari PW 719) ya saa 1.30 jioni. Mpaka anafika uwanjani KIA hakukuwa na taarifa ya kuahirishwa ama kusogezwa mbele kwa muda wa safari.



Alipoingia ndani (check-in) aliambiwa kuwa ndege hiyo sasa itaondoka saa 5 usiku kuelekea Dar. Naye aliuliza kwa nini hakujulishwa mapema ili aje saa 3 ama saa 4 akaambiwa kuwa taarifa ziliwafikia muda mchache uliopita. Akauliza, ni nani atakayegharimia ukaaji wa hapo uwanjani wakati alipanga kula chakula cha jioni Dar akajibiwa kuwa WATAANGALIA namna ya kufanya!!!



Cha kushangaza mpaka saa 3.30 hakuna taarifa yoyote ilokuwa imetolewa kuhusu chakula ama vinywaji. Alipokwenda kuuliza akajibiwa kuwa aende restaurant na alipofika huko akaambiwa kuwa hakuna chakula na wamefunga kwa kuwa walipewa idadi ya watu (cha kushangaza pengine ktk idadi hii huyu jamaa yangu hakuwemo) na hivyo hawawezi kumsaidia!



Alipokwenda kuulizia ofisini pia akaanza kujibiwa kuwa amfuate supervisor kwani hapo ofisini hawawezi kumsaidia na majibu mengine ya kejeli kuwa alikuwa wapi wakati wenzake wanakwenda kula. Mgeni wangu anasema alipofika na mpaka wakati huo hakuna mtumishi yeyote wa Precisionair aliyepita eneo alilokuwa amekaa kutangaza juu ya utaratibu wa chakula.


Haikuishia hapo...ndege ikaja wakaingia saa 5 kasorobo wakitarajia kuwa wangeondoka...waaapi! Wamendoka saa 6 na dakika 10 huku wakielezwa kuwa wanasubiri dispachi pepaz toka kwa mtu wao (PW). Swali, watu wame-check-in saa 12...alikuwa wapi huyo mtu asiandae nyaraka hizo kiasi cha kuwachelewesha wasafiri ambao walianza kupiga kelele washushwe ili waende na basi?


Katika kuingia pia kuna burudani yake kwani kulikuwa na msichana ambaye aliyekuwa akihudumia daraja la kwanza na haijulikani kama amesomea juu ya huduma kwa wateja!!!

Tunayo safari ndefu katika kutoa huduma kwa kiwango kinachotakiwa kwa kuwa inavyoonekana ni kuwa Precisionair inafanya biashara kiujanjaujanja tu. Wakati fulani nilisafiri na Precisionair toka Mwanza kwenda Kilimanjaro na kufika katikati maeneo ya Serengeti rubani akazirai ikabidi tuendeshwe na Air Hostes (Samson Mukama) akishirikiana na rubani msaidizi ambaye kwa bahati mbaya hakuwa rubani kamili bali aliyeko mafunzoni. Ilibidi rubani Kusekwa aahirishe ndege yake ya kutoka Mwanza kwenda Dar ili asaidie kutoa maelekezo kwa ‘marubani’ wa ndege yetu na tukarejea na kutua kimungumungu Mwanza.



Hivi sasa ndege nyingi za Dar-Musoma huwa zinabadilishwa bila taarifa na sababu za maana na kuwalazimu abiria kwenda Mwanza (umbali wa km 264) wakati mtu aliepuka mwendo huo.


Kama hali ya namna hii na nyinginezo za namna hiyo kampuni naweza kujikuta inapoteza wateja bure ama watu kusafiri nayo kwa kuwa hakuna mbadala…! Kwa mawazo yangu le kaulimbiu ya ‘YOU ARE WHY WE FLY’ haina maana ndani ya Precisionair.

Sunday, September 19, 2010

Sikia tu usione, utakufa kwa kihoro kama wewe ni muumini wa ile KWELI!

http://1.bp.blogspot.com/_BIB8LalXabo/TFH69O2tFHI/AAAAAAAAANA/2wmakslDhsQ/s1600/Bribe.png

Ndiyo, wakati wa kura za maoni na sasa katika mchakato wa kampeni tumesikia mengi na kuona mengi. Waliopita katika tanuru la huo mchujo watasema chini chini.

Kwamba katika kura za maoni:


Utasikia watu wanatoa rushwa lakini ukiingia UTASHUHUDIA pesa zilivyo njenje.


Utasikia TAKUKURU wanazuia na kupambana na rushwa lakini ukiingia huko utaona jinsi wanavyolinda watoaji na wala rushwa. Huko badala ya kukamata wanawambia wenzao, ‘subirini kidogo ndo mje’ ili fungu lipate kugawanywa kwanza.


Utasikia wamekamata wala/watoa rushwa lakini ukiwa humo utagundua kuwa watoa/wala rushwa hawakamatwi bali wanakamatwa ‘watu’ kwa majina kwa kufuata u-nani wao ktk jamii.


Habari toka kanda ya ziwa zinasema mtu mmoja alikamatwa na Takukuru kwa kutoa rushwa akamuuliza alomkamata ‘umejiunga lini na Takukuru? Hujui ama hujaambiwa watu wa kukamata?' Inasemekana alishushwa cheo.


Marafiki zangu wawili, mmoja wa kanda ya kaskazini na mwingine nyanda za juu kusini hawana hamu kabisa kutokana na waliyoyaona wakati wa kura za maoni na sasa wanajiandaa kutumia uzoefu wao huo kufanyia ‘thesis’ ya PhD. Hawajuani lakini wote wanasema wataangalia ‘The role of Poverty and Ignorance in Democracy’.

Ngoja nami nikapige kampeni sasa nyumbani labda naweza kupata mtaji...kama si wa kisiasa basi wa kuuza michembe…nimechoka kukaa ugenini… ;-)


Thursday, September 16, 2010

Unapokutana na watu kama hawa inapendeza, eti..eh?




Bila shaka unaikumbuka ile picha yenye kaka na dada walohusika na tukio la kuchanganya udongo wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964 ambao wanaonekana wameshika mtungi wa kuchanganyia udongo?

Basi nimekutana naye LIVE leo hapa Machame nae si mwingine ni Mama Sifaeli Shuma ambaye kwa sasa ana miaka 75 na ni mwalimu mstaafu (amekuwa Mkuu wa Shule ya Machame girls kwa miaka 20 na ushei hivi) mwenye makao yake hapa Machame Nkwarungo. Alikuwa mmojawapo wa wazee waloalikwa kwenye mkutano wetu hapa unaozungumzia mchango wa tamaduni za kiafrika katika kutunza mazingira ambao unahudhuriwa na watu toka hapa Tz, Kenya, Ethiopia, Togo, Benin, Ghana na Afrika Kusini.

Ametupa hadithi ya jinsi alivyoshiriki katika tukio hilo na jinsi alivyochukua udongo toka mkoa wa Kilimanjaro na jinsi walivyopanda mti wa mwembe kwa kutumia udongo ulochanganywa wa Tanganyika na Zanzibar hapo Ikulu na ambao mpaka sasa upo.

Bado ana nguvu na ana mchango mkubwa kwa jamii. Hii ni maktaba ambayo haijatumika kwa ufasaha na kwa kuwa pengine tuko wavivu wa kuweka kumbukumbu sijui historia yake itabakia tu katika tupicha tunatoona ama vitabu vinavyoelezea uzoefu wake.

Kama hatuna utaratibu wa kuweka kumbukumbu za watu wetu .....mmmh!

Tuesday, September 14, 2010

Ya watani wa Jadi na Prado, akina siye na VX, V8...!

http://www.autoclub.com.au/uploaded_images/toyota-gx-limited-landcruiser-prado-798309.jpg

Nimekuwa hapa kwa watani wa Jadi (Kenya) kwa muda sasa na ninashangaa kuona kuwa magari ya kifahari ni Prado. Huko kwetu ni VX na V8 sasa. Ukilinganisha gharama za Prado na V8 ziko mbalimbali sana. V8 ina gharama kubwa zaidi ya Prado.

http://www.tuningnews.net/news/080407b/delta4x4-toyota-land-cruiser-v8.jpg

Swali ni kuwa ni kwa nini matajiri wengi wa Kenya wanapenda Prado wakati wa Tz wanapenda V8? Ina maana sisi twapenda anasa kuliko watani wa jadi? Ama siye tuna hela zaidi yao?

Saturday, September 4, 2010

Huku mambo swafi nikirejea nyumbani sijui itakuwaje....!

Hapa ni stendi kuu ya matatu jijini Nairobi

Kenya kama Tanzania ina sheria inayozuia uvutaji sigara hadharani ama penye mkusanyiko wa watu.

Watani wetu wa jadi wametenga maeneo ya akina siye watundika fegi na hapo hata asokuwa na pesa anaweza kuomba wenzake pafu...lol!

Naambiwa tofauti na mnywaji pombe (ambaye ukimuomba chupa moja ya bia ama akukopeshe yeye hukadiria atakachokupa kwa ku-kalkyuleiti idadi ya bia atakazokosa...lol!), mvutaji sigara si mnyimi. Ukimuomba pafu tu anakupa papo hapo. Inasemekana kama kijana anavuta sigara na baba yake pia ni mvutaji anaweza kumgongea ishara ya kutaka fegi bila kuathiri heshima iliyopo ya baba na mwana...lol!

Laiti kama kutokuwa mnyimi huku kungekuwa katika mambo yote maishani dunia ingekuwa mahali bora pa kuishi....lol!

Tatizo langu ni pale inapoonekana kuwa watani wetu wa jadi wanajali sana suala hili kwetu ni tofauti. Ninaranda sana mitaani hapa Nairobi lakini sijamuona mtu akivuta sigara hadharani. Hata Baa kuna maeneo ya wavutaji. Huko kwetu ni nini kinashindikana?