Friday, August 27, 2010

Kisumu asubuhi hii-Mitaani ni kama wamehama!!



Leo asubuhi nimetembea mitaa ya Kisumu lakini inaonekana hakuna watu mitaani. Nauliza kunani..wananambia leo ni sherehe ya uthibitishwaji wa katiba mpya....! Mitaa ni kama inavoonekana na kama kawaida nimekutana na matangazo kama nilokutana nayo Nairobi!

Natafuta sasa dawa ya kisirani...lol! Hapo ni jirani kabisa na Kisumu Hotel inayomilikiwa na Maseno University na mbele ya Reinsurance Plaza yalipo makao makuu ya Lake Victoria
Basin Commission.

Thursday, August 26, 2010

Nimeingia Kisumu kimyakimya!!!


Nimeingia Kisumu kimyakimya. Karibuni tule kamongo na sangara.

Tuesday, August 24, 2010

Je una matatizo? Soma Hii hapa!!!!!




Miye kwa ujinga wangu nilidhani kuwa ni siye tu watanzania tunaohusudu haya mambo...kumbe nilikosea.

Katika pitapita zangu hapa Nairobi maeneo ya South 'C' nimekumbana na matangazo haya! Nilipigwa bumbuwazi na kushangaa kuwa kumbe ufahamu wa watu kuhusu mambo hayo ni mduchu!!

Sasa nadhani wenye matatizo haya tutapata usaidizi!

Kamusi ya bure:

Bibi = Mwanamke
Boma = Nyumba
Kufura mwili = Kuvimba mwili

Ajali: Kumbe hapa ni kama nyumbani pia?




Nilidhani ajali ni huko nyumbani tu kumbe na hapa ni kama kawa! Nimewahi kupata ajali ya gari mara kadhaa nikiwa abiria. Nikiri kuwa sijawahi kushuhudia ajali LIVE kama ilivotokea hii hapa Mombasa Rd mkabala na Vision Plaza :-(

Mwendesha pikipiki alokuwa anaelekea mjini (Nairobi) alimgonga mwenda kwa miguu alokuwa anakatiza toka upande wa pili na alilala bila msaada wowote. Nilikwenda kumchungulia kwa kuwa wengine wote walimuogopa na kumkuta akiwa bado anapumua...na kujifanya askari kusimamisha magari apate msaada..! Mgeni kujifanya mwenyeji kutoa msaada kwa asomjua..!


Kwa muda sasa naona kuwa barabara ya Mombasa ni mojawapo ya barabara ambazo ni BIZE ile mbaya na magari yanakwenda kasi kama vile madereva wamevuta bange...lol! Naambiwa ndo maana ya HIGHWAY...magari kwenda kasi!!!

Kaazi kwelikweli!!!

Monday, August 23, 2010

Akanambia: Nitakupeleka kwa Ukuta!!!

Niko Nairobi! Katika barabara yenye mishughuliko kibao ya Mtoni a.k.a River Road nimeingia katika duka moja kununua mahitaji. Nimenunua mpaka nimeishiwa na muuzaji wa kike ananambia kama nimeishiwa ATANIPELEKA KWA UKUTA!!!

Nimecheka sana na hasa baada ya kugundua kuwa alimaanisha kuwa atanipeleka mahali ilipo ATM machine nikapate fedha zaidi!!

Haya masuala ya lugha, kaazi kweli kweli!!

Thursday, August 12, 2010

Ametimiza Miaka Tisa!


Leo mtoto Nyamtondo Monika ametimiza miaka tisa. Pamoja na kuwa hakuna taswira yake (kwa kuwa mazingira niliyoko hayaniruhusu kuweka taswira) napenda kumtakia heri njema ya siku yake hii.

Happy birthday Monika. Dady Loves you!!!

Hapo kasindikizwa na dada Mdogo Fidelia Nkugi!

Sunday, August 8, 2010

Unapokutana na 'Principle Debater'!

Jana usiku nikiwa Kamala, nimekutana na Prof. Mbele hapa Dar. Tumezungumza mengi sana kuhusu mustakabali wa maisha yetu -kama watu na nchi- na blogging! Taarifa zingine bidae!

Alipata fursa ya kuteta kwa simu na Da Yasinta (Sweden) na pia Fadhy Mtanga ambaye amelowea Dodoma (sina hakika kama huko anachakachua kura za maoni ili waloshindwa washinde ama la!)

Monday, August 2, 2010

Vimbwanga vya matajiri!


Niko Morogoro! Jana wakati nikiwa safarini kwa basi la Mohammed Trans binafsi niliona kituko. Tulipofika shinyanga tulicheleweshwa kuondoka kwa zaidi ya nusu saa kwa kile tulichoelezwa kuwa kuna bahasha toka kwa mkurugenzi wao wanayopaswa kuondoka nayo na gari haliondoki mpaka ije!

Maswali mengi: mpaka gari inatoka Mwanza ikafika Shinyanga hakuwa na mawasiliano na gari hilo?
Kipi bora: bahasha kwenda huko inakokwenda ama abiria wanaomfanya aitwe mkurugenzi?


Anyway, Mt. Simon tuwasiliane....kama uko Morogoro tuonane...lol!