Saturday, July 31, 2010

Msimu wa Jando na ukeketaji umewadia!!!


Leo hii wamepita vijana watatu wakiwa na ngoma ya kinyeji kwa wakurya na jamii zake zote ya Rirandi wkiwa mitaani eneo la Old custom road wakijivinjari. Hiyo ni dalili kuwa kesho watakatwa (watapashwa tohara).

Zamani ilikuwa unawaona na mabinti wakiwa kwenye msafara lakini siku hizi kwa kuwa kuna sheria ile ya SOSPA (sexual offenses special provision act) hawarandi mitaani. Wao hung'olewa (hukeketwa) kimyakimya!! Utaona vibinti vikiwa vimejifunga kanga na vinatembea kama bata unajua tu KESHALIWA huyo(msemo wa Da Yasinta na Da Koero: Ukiona Manyoya jua keshaliwaaa!!!).

Kinachoshangaza ni kuwa pamoja na kuwepo kwa sheria hiyo bado mambo ya ukeketaji yanaendelea. Kuna mambo mawili ama matatu: Moja ni kuwa kuna watu wanashindwa kutimiza kazi yao; watu wanang'ang'ania mila isiyofaa ama waliotunga sheria hawakufanya homework vizuri.......waweza endeleza mlolongo huo!!

Ipo kazi, wanaharakati wanasema ukeketaji kwa wanawake ni mbaya. Mbona wanaopiganiwa hawaonekani kuujua ubaya huo?

Friday, July 30, 2010

Kuna ugeni huku

Dr Slaa anatarajiwa kuingia Musoma wakati wowote ule kuanzia sasa.

Mji wa Musoma umezizima.

Wednesday, July 28, 2010

Hatimaye walojifukia watoka shimoni

Hebu tazama maluweluwe haya hapa Jamii Forums. Nitarejea baadaye ngoja nipate supu ya pweza kwanza.

Kuna maswali magumu ya kuuliza kabla ya kuwa hewani!!!!

Musoma tumefulia?



Barabara ya Nyerere mjini inavoonekana usiku. Kuna taa za mtaani ambazo haziwaki ikiwa ni pamoja na kwenye ile barabara ya kuelekea eapoti mpaka RC conference centre.

Zilizoko kwenye barabara ya Mukendo nazo zinawaka kwa kusuasua. Jambo la kushangaza ni kuwa kwenye taa hizo kuna mabango ya Tigo na Zain ambapo hayo makampuni yanalipa gharama za matangazo kwa kila nguzo.

Cha ajabu zaidi wakubwa wakija taa hizo zinawaka. Tatizo ni zain, tigo ama manizubaa?

Mmmhh!

Thursday, July 22, 2010

It is a joke!! Lakini unapotaka kikubwa zaidi ya unachopaswa kupata kitakugharimu!!!

Wakandarasi watatu walikuwa wanatembelea mbugani. Mmoja alikuwa anatoka Botswana, mwingine kutoka Rwanda na wa tatu kutoka Tz. Baada ya kutembelea mbuga na mapumziko meneja wa hoteli waliyofikia akawauliza kazi wanazofanya huko walikotoka.

Wakamjibu kuwa wao ni wakandarasi na meneja aliposikia hivyo akawaambia 'tunahitaji kukarabati mojawapo ya uzio huko nyuma ya hoteli. Kwa nini msiuangalie na kisha mnipe makisio ya gharama za ukarabati?' Wakandarasi wote watatu wakiongozana na meneja wa hoteli wakaelekea huko nyuma kwenye uzio.

Aliyeanza ni mkandarasi kutoka Botswana ambaye alichukua futi-kamba na penseli. Alipima na kisha kufanya mahesabu yake na kumwambia meneja 'nadhani kazi hii itafanyika vema kwa gharama ya dola 9000 ambapo dola 4000 ni kwa ajili ya vifaa, dola 3000 kwa ajili ya mafundi na dola 1000 kwa ajili yangu kama faida itokanayo na kazi'

Wa pili kutoka Rwanda naye alichukua futi-kamba na penseli na kufanya mahesabu yake. Majibu yake yalikuwa ; 'kazi itafanyika vema kwa gharama ya ya dola 7000 ambapo dola 3000 zitakuwa za vifaa, dola 3000 kwa ajili ya mafundi na dola 1000 kwa ajili yangu'.

Bila kujishughulisha mkandarasi toka Tz akasema 'dola 27,000'.

Meneja alishangaa sana huku akimtizama mkandarasi toka Tz akasema, 'hukuchukua hata futi-kamba kama wenzako. Inakuwaje umepata kiasi kikubwa namna hiyo?'

Mkandarasi toka Tz akasema, 'aah!! mbona rahisi tu? Dola 10,000 kwa ajili yangu, dola 10,000 kwa ajili yako (meneja) na kwa ukarabati tunamkodisha Mnyarwanda kutufanyia kazi!'

Kama kichekesho hiki kina ukweli yaweza kuwa ndo sababu mambo yetu hayendi kama tunavotarajia?

Monday, July 19, 2010

Uchafuzi wa mazingira-nani ni nani?




Kila asubuhi na jioni mambo huwa kama hivyo katika kiwanda cha nguo cha Mutex!!! Moshi mzito mweusi kama lami... :-(

Kwa maana hiyo asubuhi wale walioko eneo la magharibi huipatapata wakati wa jioni maeneo ya mashariki nao huipatapata.

Aidha wananchi ama serikali wamelala! Watakapoamka itakuwa too late!

Mapumziko na kilimo kwanza!

Nilikuwa na mapumziko katika shamba la watawa la Baraki wilayani Rorya wikiendi nzima. Tukawa kanisani Jumapili


Kisha kukawa na mapokezi ya trekta kutoka Arusha lenye thamani ya zaidi ya Tshs 50m kwa ajili ya kutekeleza kwa vitendo!


Saturday, July 17, 2010

Breaking News: Kamala kuwa Baba soon!!!

Habari zilizonifikia ni kuwa ndugu Kamala anatarajiwa kuwa baba leo. My waifu wake alipatwa na uchungu usiku na kupelekwa hospitali ya Mugana kwa ajili ya kujifungua.

Tutawajuza punde.

Tunamuombea ajifungue salama.

Thursday, July 15, 2010

‘Vijana waache kutumiwa’


JINA LA KAMALA si geni kwa wanablogu wengi. Yeye ni mwendeshaji wa blogu maarufu inayojadili (pamoja na mambo mengine) masuala ya kiutambuzi. Bonyeza hapa kuitembelea. Ndugu Kamala anajulikana pia kwa namna yake ya utoaji maoni huru katika blogu anazozitembelea ambayo hufikirisha na mara nyingine kuibua mijadala mijadala zaidi.
Blogu hii ilipata fursa ya kuzungumza naye siku chache zilizopita kuhusu falsafa zake, blogu, dini, siasa na mambo yake binafsi. Karibu kujua zaidi kuhusu mwanablogu huyu anayeblogu kutokea kanda ya ziwa.

________________________________________

Ndugu Kamala, nashukuru kwa kukubali kutumia muda wako ili tuweze kujadiliana masuala mawili matatu. Labda tuanze na falsafa yako binafsi. Unaamini nini katika maisha ambacho ndicho kinachobeba utambulisho wako kama Kamala?

Naamini katika utu, ubinadamu, upendo na umoja. Napenda kuelewa vitu na kudadisi na ndio maana natumia majina ya kihaya tu ninayoelewa maana yake na kwa nini yawepo… napenda kuacha maisha yaende na kufurahi muda wote

Falsafa nzuri. Umetoa mfano wa majina ya kihaya kwa dhana ya udadisi. Nini tafsiri ya majina yako mwenyewe? nakumbuka kuna siku ulisema mahali, ila pengine wapo wasomaji hawapata maana hiyo kule….

Kamala maana yake ni msuluhishaji, anayeyamaliza. Lutatinisibwa ni jasiri asiyetishika, jina hili limeongezwa madoido kadhaa ambayo hata hivyo siyo ya msingi saaana ila kama ulivyo utamaduni wa wahaya hupenda kujisifia na kujikweza. Lutabasibwa ni jasiri mwenye nguvu asiyewezekanika.

Bila shaka maana yake, huwezekaniki na ni jasiri. Tuje moja kwa moja katika suala la blogu zetu. Unasoma blogu ngapi kwa siku/wiki?

Kwa kweli sina idadi kamili…nasoma blog nyingi kufuatana na muda au ufikiwaji. Kwa hiyo najitahidi kusoma nyingi sana niwezavyo kwani napenda kupitia, ila napenda blogu zenye kufikirisha zaidi na zile za mambo ya kiroho na utambuzi

Kwa faida ya wanablogu, unadhani tunawezaje kujikita katika kufikirisha zaidi katika hali ambayo utamaduni wa kufikiri haujawa sehemu ya jamii yetu (yaani tunapenda kusoma habari nyepesi nyepesi zaidi)?

Ni kwa kutokuwa na upande na kuwa na maoni yetu. Kusimamia tunayoyaamini bila kufungwa na upande wowote…kuwa watu wa kijifunza kwa kusikiliza sana na kupenda kujifunza kutokana na mazingira; kusikiliza maoni na mitizamo ya wengine…kujisomea na kuwa na tabia ya kudadisi na kuhoji. ni lazima kuwa wabunifu. Tunahitaji kuwa watu wa kusimamia ukweli wa fikara zetu hata kama ni mchungu kwa wengine au kwetu pia.

Mara nyingine umekuwa ukipotea potea kwenye kijiwe chako pale. Je, ni makusudi?

Sio makusudi. Ni kwa sababu ya safari yaani kuwa mbali na mtandao lakini na wingi wa shughuli za kila siku…huwa nasikitika kwahilo.

Tumeona sasa wanablogu wameanza kukutana. Juzi hapa wapo wenzetu watano walifanikiwa katika hilo. Je, kuna mwanablogu yeyote umewahi kukutana naye uso kwa uso tangu umeanza kublogu? Ilikuwa wapi?

Nimekutana na wanablogu kadhaa kwa nyakati tofauti kama vile Kaluse, Dalali, Tandasi, Mjengwa wote jijini Dar Es Salaam, lakini nimekutana na Chacha Wambura, Strictly Gospel mjini Musoma kwa wakati mmoja mwezi April 2010. Nafanya juhudi za kuwasiliana na wengine na ndio maana niwapo katika mji wowote huwa najitangaza ili kama wapo tutafutane na napanga kufanya juhudi zaidi za makusudi.


Hapa akiwa na mwana wa mwanablogu mwenzetu | Picha kwa hisani ya Kamala

Safi sana. Hongera kwa kukutana na wanablogu wengi kiasi hicho. Kwa idadi ya blogu za Kiswahili tulizonazo mpaka sasa, unadhani tumepiga hatua yoyote? Kwa kiwango gani?

Hatua tuliyopiga ni uhuru wa mwandishi kutoa habari aliyonayo. Kwa hiyo kila mwenye blogu atakacho kutoa hukitoa bila urasimu wowote na hivyo uhuru wa maoni au habari upo japo kiwango bado kinakutana na ukosefu wa internet kwa wa-Tanzania walio wengi ila angalau taarifa zinaandikwa na historia zinarekodiwa.

Je, unadhani blogu zetu zina upungufu wowote ule? Kwa maoni yako, tunawezaje kuboresha zaidi blogu zetu.

Tunahitaji kuamini katika uhuru zaidi wa kuwa huru bila kuegemea upande, tusitoe kibubusa (dogma) bali tuwe huru na kuvutia wasomaji huru ili kuleta dhana ya uhuru wa maoni. Tujisikie kuwa na deni kwa wasomaji wetu na hivyo tuache kupotea kwenye blogu zetu, tujitahidi kuwepo kwani wasomaji wanatutegemea.

Tuje kwenye blogu yako mwenyewe, nini hasa falsafa kubwa/kipaumbele cha blogu yako?

Ni kujitambua, kuleta mawazo huru, kujiuliza maswali magumu na kuleta mfumo mpya wakufikiri na sio kuacha watu wachache watusaidie kufikiri.


Kuhusu mfumo huo mpya wa kufikiri unaoungolea, wapi pa kuanzia?

Kujitambua, kujibainisha, kujua nafasi yetu na kutokuwaachia watu wengine watusaide kufikiri. kudadisi na kuhoji kila jambo. Kuwa na mada zenye kufikirisha zenye kuleta mitizamo mipya na zinazochokonoa fikra zaidi kwenye blogu zetu. Ni lazima tutizame mambo katika uhalisia wake. Tahajudi yaweza kusaidia katika hili.

Una maoni gani kwa anonymous na dhana ya uhuru wao maoni? Kuna watu wanakuwa na mashaka na umuhimu wao katika blogu; wanasema kwa nini mtu mwenye mawazo yanayojenga akimbilie kujificha kwanza ndio aseme? Una maoni gani na hili...

Anony!! kuna wakati wanaonekana kuchanganya au kakera na hata kushangaza labda, Lakini unaposema maoni yanayojenga, unamaanisha nini?? nani mwenye mamlaka ya kujua kuwa maoni fulani yanajenga??mtoa maoni (akiwemo anony) au msoma maoni (mwenye blogu)?? Lakini je, wewe hujawahi kuwa anony?? Naamini katika uhuru wa maoni na hivyo ni vigumu sana kwangu kumsemea mtu. Kwa hiyo ma-anony pia wa uhuru wao na kuna umuhimu wa kuwa anony wakati mwingine. Bila shaka ma-anony wanajisikia huru wakiongea yale wayaongeayo.


Sawa sawa. Nadhani ujumbe umefika. Je, ulianzaanzaje kublogu?

Niliona blogu za kiswahili nikiwa mwanafuzi wa computer science (sayansi ya tarakilishi) mwaka 2006 nikaamua kujifunza kutengenza blogu na ndo nikaanza kublogu.

Oh, kumbe kitaaluma wewe ni mtaalamu wa computer. Hongera sana. Unawasaidiaje wanablogu wasio na taaluma yako katika kuboresha nyenzo za blogu zao?

Kuwasaidia wengine??? naomba nisijisemee ili kuzuia changamoto za kihaiba (ego) kuingilia nafasi yangu ila kumbuka kuwa msomi wa computer sio kigezo pekee au muhimu cha kujua kublogu, kutengeneza blogu na kuziendesha kwani hata ukiangalia blogu yangu utaona mapungufu kibao, niko bize. Lakini kuna wanablogu wengi ambao nimesaidiana nao katika kuingia kwenye tasnia hii, naomba nisiwataje

Mara nyingi umezungumzia mitazamo mibovu unayoiona katika jamii yetu. Unadhani ni hasa chanzo cha mitazamo hiyo?

Chanzo ni kibubusa, yaani kuacha watu watusaidie kufikiri, kutokujitambua na kutotafuta mitizamo mipya

Una mtazamo gani kuhusu dini na jamii?

Dini na jamii ziweze kufanya yale zinazoyafundisha lakini ziwe dini za ukweli na sio dini za kugombanisha watu wala kuwatenga…ziwe dini za kuunganisha binadamu si za kuleta vurugu.Ila naona kama dini zetu tulizonazo ni za kuepuka kama tunataka kwenda mbele. Natamani watu waone tofauti iliyopo kati ya dini na waanzilishi wake. Pia kati ya dini na vitabu vya dini hizo (misaafu)… pia kati ya vitabu hivyo na waanzilisha wa dini hizo, waanzilishi wadini na Nguvu Kuu (Mungu?). Tunahitaji uhuru katika dini, uhuru wa maoni na mitizamo na si kikwara ya kukufuru nk au kwenda motoni. Dini zisiegemee kutoza fedha tu bali kuleta mabadiliko.

Je, u muumini wa dini yoyote kati ya hizi maarufu zilizopo?

Dini zipi zilizopo?? Inawezekana kuna dini usiyoijua. Ila nilipokuwa Dar nilikuwa nikienda kanisani na kuimba kwaya…ila nilipohamia mikoani naona kama maji yako shingoni. Lakini mimi naamini katika dini ya upendo na heshima kwa kila kiumbe hiyo ndiyo universal religion ninayoiamini. Hata hivyo, ni lazima tujue au tukumbuke kuwa dini zoote huongelea kitu kile kile kwa lugha tofauti, mazingira tofauti na tamaduni kutokana na uanzilishi wake. Ukiunganisha mafundisho ya dini hizi zoote, utapata universal religion ambayo ndiyo ninayoiamini.

Una maoni yoyote kwa vijana wa kizazi cha leo katika Tanzania?

Vijana ni lazima wajitambue, watafute utume wao na kuutumikia, ni lazima wajue ya kuwa wapo hapa (kwenye miili) kwa lengo fulani na ni lazima walitimize lengo hilo. Ni lazima washike mienendo yao mipya. Vijana wanapaswa kujua ya kuwa jamii yote inawategemea yaani watoto na wazee. Ni lazima waache kutumiwa na ni lazima watambue nafasi zao katika jamii…vijana wanapaswa kujua ya kuwa ujana ni wakati muhimu sana kwamba kila ugunduzi au ukombozi huletwa na vijana. Ni lazima wafanye kazi kwa bidii lakini ni lazima wajue nafasi zao. Lakini wajue kuwa ujana unapita na wengi wanatamani kurudia ujana kwa hiyo wauishi ujana wao wasijetamani kuurudia pale utakapokuwa umepita.

Ukizungumza kwa mifano binafsi: una utume gani hasa ambao wewe binafsi unautumikia? Unatumiaje ujana wako Ndugu Kamala…

Duhu! kujisemea ni tatizo ila ninaelimishana na vijana katika mambo mbali mbali ya kiutambuzi, ujasiriamali, siasa na yale ya kijamii. Ninapeana ushauri mbali mbali na kujifunza mengi kutokana na vijana wenyewe.


Mwisho tumalizie kwa maisha yako binafsi. Unajishughulisha na nini Kanda ya ziwa? Vipi mwamko wa blogu huko?

Kanda ya ziwa naishi, nablogu, nalima, naandika, natafiti, nahamasisha, ni fundi, ni kiongozi wa familia, mwanaharakati, ni mwanamazingira, mshauri, mwanautambuzi nk nk. Mwamko wa blogu sijui ila juhudi zahitajika kuuamsha.
Bila shaka utakuwa wa kwanza kumsha ari hiyo kwa kipindi utakachokuwa huko. Hakuna mwanablogu yoyote uliyeonana naye ukiwa huko?
Nimeonana na kuwasiliana na mmoja wao na wengine. Ni kweli najaribu kuamsha ari lakini bado ni changamoto iliyoko mbele yangu...


Pichani Kamala katika pozi |Picha kwa hisani yake mwenyewe

Una kipi ambacho ungependa kuwaambia wasomaji wako ambacho unaamini hawakijui kabisa kuhusu wewe?

Labda ni migogoro kati yangu na familia yangu (niliyotokea). Kwamba pamoja na utambuzi niko mbali na wanafamilia woote, sielewani nao. Ni familia ya kilokole lakini ndugu na ndugu hawaongei au mzazi na mwana pia hawaongei.

Pole sana kwa hayo. Je, umejaribuje kuitumia elimu ya utambuzi kuleta mabadiliko kwa wanandugu hao?

Ki utambuzi kuna watu tu. Mambo ya ndugu, rafiki jamaa nk, ni vibandiko vya ziada. Lakini pia ninao ndugu wengi sana ukiwemo wewe na wengine. Kwa hiyo, hali hii kwangu ni furaha, ni faraja na nafurahia…maisha yanaendea ni changamoto nzuri za kufanya maisha yawe na maana zaidi


Nakushukuru sana kwa mazungumzo haya. Bila shaka yamewapa fursa wanablogu kupata mengi zaidi kuhusu wewe. Asante sana Ndugu Kamala.

Asante pia kwa kuniuliza maswali haya, naamini hii ni sehemu ya mafanikio ya blogu yangu. Nashukuru sana.

Asante sana kaka.

Hii nimeidesa kwa kaka Bwaya

Monday, July 12, 2010

Tunao Maadui wangapi?

  • Wakati tunapata uhuru tuliambiwa kuwa tunao maadui watatu: Ujinga, umaskini na Maradhi.

  • Miaka 45 sasa bado maadui hao wapo na inaonekana kuwa wameshajenga kibanda na hivo tutaendelea kuwa nao ndani ya kaya hii ya wadanganyika!

  • Kwamba sasa inaonekana kuwa mbali na madui hao watatu kuna wawili wameongezeka na naambiwa kuwa ni UFISADI na RUSHWA.

  • Kwamba pamoja na kuwa na nyenzo za kupiga vita maadui hao lakini bado mambo yako palepale!

  • Kuna wanaodhani kuwa sasa tunapoambiwa kuwa kuna mkakati wa kukuza uchumi na kupunguza umaskini Tanzania (MKUKUTA) badala yake ni kuwa kuna mkakati wa makusudi kabisa wa kuongeza umaskini na kuondoa uchumi (kuhamisha rasilimali -mazao ya uvuvi, mazao ya misitu, madini n.k. nje ya nchi) Tanzania.
Ninawaza kwa sauti tuwaungwana!!!

Friday, July 9, 2010

Wikiendi njema na tafakari ya picha hii!

Inasemekana madhiwa ya mama kwa ntoto ndo chakula bora kuliko zote. Inakuwaje sasa wanaofaidi ni baba zao huku watoto wakiishia kula madhiwa atifisho?

Nawaza sana!!!

Friday, July 2, 2010

Uzee dawa ati!



Uzee kitu adhimu, huo ninauingia
Ujana sasa adimu, Shabani aliusia
Maungoni mwangu humu, uzee unanijia,
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Mbali ninamuachia, rafiki yangu ujana,
Miaka inakimbia, ya leo siyo ya jana,
Nabaki nakumbukia, nilipokuwa kijana
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Shabani aliandika, kaulilia ujana,
Ni vipi unamtoka, kashindwa kuung’ang’ana,
Meno yalimdondoka, na nguvu tena hamna,
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Taratibu waingia, uzee wabisha hodi,
Siwezi kuukimbia, hata niwe mkaidi
Hata nikitukania, ndivyo napigwa baridi,
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee

Mvi sasa zanijia, nimejaribu kung’oa
Kidevu zasalimia, na miye nazichomoa,
Nikitoa zazidia, nami nazidi kutoa!
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Mapensi nayaachia, na macheni ya shingoni,
Hereni nilivalia, kwenye sikio jamani,
Mwendo nilibadilia, nilivyonesa njiani,
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Niliwapata mademu, tena wengine kwa zamu,
Nikaitwa mtaalamu, wa mambo yale matamu
Sasa yanitoka hamu, nanyimwa hata salamu!
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Nilenda nilipotaka, wasiponitaka nilenda,
Sikuwa na hata shaka, ati mtu kunidunda,
Leo naogopa paka, ninavutwa kama punda,
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Mwendo wa kudemadema, nikishika natetema,
Uso umenikunjama, natembea nikihema,
Magoti nayo yauma, uzee si lele mama!
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Kumbe maisha ni hivi, uzee haukwepeki,
Ninazikubali mvi, hata kama sizitaki,
Uzee siyo ugomvi, ujana haushikiki,
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Kweli nilifurahia, enzi zile za ujana,
Kamwe sintoyarudia, yalopita naagana,
Uzee nakumbatia, kwani lingine hakuna,
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Nasubiri wajukuu, nione na vitukuu,
Nakunja miguu juu, na mshukuru Mkuu
Kuona umri huu, enzi hizi ni nafuu,
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Na. M. M. Mwanakijiji
(Sauti ya Kijiji a.k.a Vuvuzela Matata)


Shairi hili nimelidesa kwa Michuzi