Sunday, June 27, 2010

Nafikiria kutangaza Nia!!!!



Nimewasili Dodoma. Ngoja nile zabibu na ubuyu labda ntapata akili ya kutangaza nia kabla sijaondoka hapa!

Nikitangaza hapa itakuwa safi kwa kuwa nikitangazia kwingine ntaitwa vuvuzela!!!

Hivi ni kwa nini hasa vyeo hivi vya ubunge vinaonekana ni vya watu ama tabaka fulani?

Friday, June 25, 2010

Tunapoingia kwenye biashara tunajua tunalolifanya ama ni kufuata mkumbo tu?



Majuzi (jumapili ilopita) nilipokuwa natoka Mugumu Serengeti kuja hapa Arusha tukiwa tunakaribia kijiji cha Park Nyigoti tairi ya mbele upande wa dereva ya basi la KIMOTCO ilipasuka. Bahati yetu tulikuwa ndo tunamalizia mlima kukamata mteremko wa kuitafuta Fort Ikoma!!!!!!!!


Tulibadilisha tairi na kuondoka kuelekea Arusha. Njiani ikawa mara paipu ya upepo imelegea, mara mafuta hayapandi n.k.


Tulipofika Karatu ikabidi kufungua paipu za mafuta na kwenda kuchomelea kwa gesi na badala ya kufika saa 11 ama 12 tukaingia Arusha saa 2 usiku tukiwa tumechoka ile mbaya.

Lazima niwe mkweli na isieleweke kuwa nawapiga vita. Kusema ukweli kati ya makampuni yenye magari mabovu yanayofanya safari kati ya Musoma na Arusha kupitia Serengeti ni KIMOTCO. Wenzao wa COAST LINE na ZAKARIA wanajitahidi. Ukipanda KIMOTCO ujue kuwa kufika kwako Arusha ama Musoma siku hiyo ni bahati nasibu.

Nakumbuka siku moja tukiwa Arusha tumeondoka saa 4 asubuhi badala ya saa 11.45 asubuhi tena baada ya kumpigia simu kamanda wa polisi wa mkoa wa Arusha.

Hebu fikiria, mtu ameamka saa 9 usiku na baridi la Arusha kuwahi basi na haondoki mpaka saa 4 inakuwaje?

Swali hapa ni kuwa je watu wanapoingia katika biashara wanakuwa wanjua wanachokifanya ama ni mkumbo tu?

Aaaagh!

Tuesday, June 22, 2010

Kukutana na aliye Mbali katika huzuni!

Leo jioni nimekutana na Prof. Matondo katika kituo maarufu cha Dannish hapo Usa River Arusha. Ni mkutano ulotukutanisha akina siye ambao hatujawahi kukutana mbali na kukutana mtandaoni.

Hata hivyo, Prof. Matondo yuko katika wakati mgumu kwa kuwa amepata msiba wa Mpwawe ambaye pia alikuwa anasaidia kumwangalia Mama Matondo. Mpwawe hyo alifariki leo asubuhi baada ya kuugua kwa muda mfupi!

Ni kipindi kigumu sana kwa mwenzetu huyu. Tunamwombea kheri na ustamihilivu katik kipindi hiki pamoja na magumu yanayomkabili.

Kuonekana kwangu hapo alipokuwa ilikuwa faraja fulani na pia alipata nafasi ya kuongea na kaka Kaluse kwa simu.

Picha mtazipata baadaye!

Saturday, June 19, 2010

Picha mnato-Ajali



Leo mchana nikiwa naelekea Serengeti kupitia Nyamongo (North Mara) nimekuta ajali hii ilohusisha gari aina ya Ford stationwagon katika kijiji baada ya Mogabiri. Inasemekana dereva alikuwa anakwepa ng'ombe na mwenda kwa miguu na kwa vile alikuwa 'mafuta' alikosa mwelekeo na hivo akapinduka na kubiringika mara 3 kisha gari likatazama lilikotoka (Nyamongo) huku likiwa chali. Dereva alipona lakini, mwenda kwa miguu (mdada) alikuwa analalamika maumivu ya nyonga/kiuno.

Madereva twendesheni kwa uangalifu wajameni!

Leo Ni Hepibesidei Yangu!

Jamani leo mie ni mtoto! Ninadeka kweli leo!

Wakati ninafikiria hivi najeiweka chini ya nguvu kuu (Mungu) ili niweze kupenda na si kupendwa, kusikiliza na si kusikilizwa na kuleta matumaini pale palipo na madhila.

Tuesday, June 15, 2010

Barua ya Wazi kwa Mke Wangu Mpendwa!





Kutokana na kuamini kwangu juu ya utakatifu wa ndoa na umuhimu wa kuitenga na kila kitakachoivuruga au kuichafua;

Nakutumia nasaha hizi kutoka moyoni, juu ya namna tutakavyoishi katika kipindi cha mashindano ya mpira ya Kombe la Dunia; Ili tutoke na madhara machache kadri inavyowezekana...

Na hizi zifuatazo ndiyo nasaha za mumeo mpendwa:


1. 1: Katika kipindi cha kuanzia tarehe 11 Juni mpaka tarehe 11 Julai njia pekee itakayokuwezesha kufungua mazungumzo kati yetu ni kuwa ufuatilie magazeti ya michezo na habari za kombe la dunia. Na ni kwa njia hii tu itaniyumkinia kushiriki nawe katika mazungumzo na majadiliano... Na utakapoleta maongezi mengine yoyote nje ya mada ya Kombe la dunia basi nitalazimika (nasikitika kusema) kutokujibu, na hili ni jambo ambalo litakalo kuudhi.

2. Na katika kipindi hiki cha kombe la dunia TV itakuwa ni mali yangu kwa muda wote. Na nikikuona unaiangalia Remote Control, basi utapoteza moja ya macho yako mazuri.

3. Kama utataka kupita mbele ya TV wakati wa mechi, au kabla yake au baada yake, mimi sitokuzuia, endapo tu unapita huku unatambaa kama komadoo wa jeshi wakati wa vita kuu ya dunia.

4. Wakati wa mechi ni lazima utambue kuwa mimi sisikii wala sioni na wala siongei, isipokuwa kama nitahitaji chakula au kinywaji, na sitokubali kusikia maneno kama vile; jibu simu, au katuletee hiki kutoka dukani au kafungue mlango...

5. Kama utatekeleza hayo hapo juu basi nitakuruhusu kuangalia TV kuanzia saa 8 usiku mpaka saa 12 asubuhi kwani hakuna kipindi kitakacho nihusu...

6. Nakuomba, kasha nakuomba na tena ninakuomba sana mke wangu, tafadhi usiniambie maneno yako ya kunipoza kama vile eti huo ni mchezo tu, au eti watashinda mechi nyingine, kama utaniona nimehuzunika kwa sababu timu ninayoishabikia katika kombe la dunia imepoteza mchezo, kwa sababu hayo maneno yako hayatonisaidia bali huenda yataniongezea hasira na uchungu na yanaweza kusababisha mmoja wetu kulazwa hospitali na mwingine kufungwa jela...

7. Sina kikwazo kama utakuja kuangalia mechi pamoja na mimi, na nitakuruhusu kuongea wakati wa mapumziko endapo tu matokeo ya mchezo yanaelekea kuwa mazuri kwa timu yangu. Nakuomba upigie mstari swala la matokeo kuwa mazuri.

8. Marudio ya magoli katika TV ni muhimu sana kwangu na sina tabu hata kama nitaliangalia goli moja mara 100, usishangae.

9. Katika muhtasari wa kila siku wakombe la dunia sitaki kusikia unasema mechi umeshaiona, kwa nini unaangalia tena muhtasari. Jibu langu litakuwa: angalia namba 1 na 2 za barua hii.

10. Baada ya fainali za kombe la dunia nakuomba usiseme Alhamdulillah kwamba kombe la dunia limekwisha na halitokuja tena mpaka baada ya miaka mine, kwa sababu maneno kama hayo hayana nafasi katika kichwa changu. Nakuomba usisahau kuwa kuna kombe la Euro, Euoropean Championship, Europa, English Premier League, FA Cup, Ligi kuu ya Spain, Italy, n.k. Hivyo naweza kuamua kwa wepesi kabisa kulipizia kile nilichokikosa katika kombe la dunia

Nakushukuru mke wangu kwa kunisikiliza na kukubali kushirikiana nami katika hili.

Mumeo mpendwa ...

Chanzo: Mtandao wa upashanaji habari wa www.thefoundation-tz.org

Friday, June 11, 2010

Nani atamaliza dhana ya MKUKUBI!



Ina semekana kuwa Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania (MKUKUTA I) umeshindwa kutimiza malengo yake na sasa tunaingia MKUKUTA II ikiwa na malengo yale yale na imerithi changamoto za MKUKUTA I.

Inasemekana kuwa watanzania tulio wengi tunapenda sana semina, warsha, makongamano na mikutano hasa yenye kutoa BAHASHA. Bahasha hiyo imegeuzwa jina na kuitwa Mkakati wa Kuondoa Umaskini na Kukuza Uchumi Binafsi (MKUKUBI)!!!!!

Ndiyo, nimeshuhudia watendaji wa serikali na NGOs wakiitwa ama kwenda kwenye mikutano ama warsha wanauliza kwanza 'mnalipa kiasi gani kwa siku?' :-(

Nimewahi kusikia kuwa on average kuna watendaji wa serikali na NGOs wasoenda field badala yake hukimbizana huku na huko kwenye mikutano yenye MKUKUBI na huhudhuria mikutano zaidi ya 300 kwa mwaka!

Kwa bahati mbaya ujinga huu umeambukizwa mpaka kwa wanakijiji na usipotoa mkukubi kwenye vikao vya kuzungumzia maendeleo watakususia kikao na vingine utakavyoitisha.

Nimeshuhudia watu wakikacha mikutano hata ile yenye kutoa elimu juu ya mambo mbalimbali kwa kuwa ati hakuna mkukubi.

Inasemekana mkukubi uliletwa na wadau wa maendeleo (donors).

Tofauti na akina siye, uzoefu toka kwa watani wetu wa jadi (KENYA) ni kuwa wao hulipia kwenda kwenye mikutano ya aina hiyo hiyo hasa pale wanapoona kuwa ina manufaa kwao wenyewe na kwa jamii wanayoiwakilisha.

Tutabadilika lini?

Nani wa Kuanzisha mwendo?



Kuna tangazo redioni lililodhaminiwa na Champion.
Baba analalamikia mapishi ya mkewe kuwa ni maharagwe tuu habadilishi. Mama anamlalamikia baba kuwa yeye akitoka kwenye ugimbi na ndizi choma haina kitu zaidi, hata chachandu!

Mama anajitetea kuwa hakujua kama baba anataka mabadiliko na kufundishwa kupika samaki wa kupakwa. Baba naye anajitetea kuwa hakujua kama mama anahitaji saaaana chachandu kwenye ndizi choma.

Swali ni: Nani anaanzisha mazungumzo? Baba ama mama? Ama ni utamaduni kuwa ni lazima baba ndo aanzishe mazungumzo?

Wednesday, June 9, 2010

Kama kuna ukweli basi kazi ipo!

Katika kipindi kilichooneshwa TBC1 leo majira ya saa tano asubuhi kijulikanacho kama "UA LETU" (sina hakika kama kilikuwa kinarudiwa ama kilikuwa kinarushwa kwa mara ya kwanza) Mtangazaji Suzan Mungy alikuwa anawahoji watoto, walimu na wazazi wa pahala ambapo wanafunzi walikuwa wanadondoka hovyo shuleni huko Dodoma.

Imepelekea baadhi ya watoto kupelekwa katika kituo cha Ukombozi kwa ajili ya maombezi. Katika mahojiano na Mchungaji Christine Bahati wa kituo hicho alisema kuwa katika kuwaombea walikutikana na MAPEPO kwa kuwa mapepo huwa yanpenda kuwavagaa watoto kwa kuwa ati yanajua kuwa miongoni mwao watakuwa pengine Rais, mawaziri, wabunge, wakuu wa mikoa, wahadhiri, wakuu wa wilaya, wanasheria n.k.

Kwamba katika kuwavagaa wanawafanya wawe na roho ya kishetwani na kufanya madudu ukubwani. Na hivo wanahitaji kuombewa wakiwa watoto ili wasijekuwa viongozi/wazazi/raia wabaya ukubwani.

Kwa dhana hiyo nikitafakari kauli ya mchungaji na kujirejesha kwa yanayotokea kwenye jamii yetu na nchini kwa ujumla nachelea kusema pengine viongozi wetu tulionao wengi walivagaliwa na mapepo walipokuwa watoto :-(

Ni wazo tu linanisumbua

Tuesday, June 8, 2010

Sheria ya Madini 2010: Tunakusubiria Mkuu!

Jk akisaini sheria ya matumizi ya fedha za uchaguzi

  • Kwa kawaida wenye kumiliki rasilimali za nchi ni wananchi na si kikundi kidogo cha watu kilichoko katika ngazi za maamuzi kama chama ama serikali.

  • Kwa kawaida wenye mali huwateua baadhi ya watu kuwasaidia kumiliki mali hiyo kama kampuni (ya ndani ama kigeni), wizara ama idara ya serikali.

  • Kwa kawaida wenye mali wanayo haki ya kujua jinsi mali yao inavyowaletea faida na wanapaswa kuiona faida hiyo kwa macho na si kwa kuambiwa kwa maneno na kusoma mafao hayo magazetini ama vitabuni.

  • Kwa hiyo tunahitaji sasa kujua hatma ya rasilimali zetu toka kwa tuliowapa kazi ya kutuwakilisha kuitunza na kuhakikisha kuwa inatuletea manufaa na si madhara ama kutuongezea umaskini.

  • Tumeshuhudia sheria ya matumizi ya fedha katika uchaguzi ikipitishwa haraka na kusainiwa haraka. Pamoja na mapungufu yalioyojitokeza tunasema bravo kwa uharaka huo wa kutenda.

  • Tumeshuhudia mswada wa sheria ya madini ya mwaka 2010 ukipelekwa bungeni kwa staili ya "Certificate of Emergency" na ukapitishwa kuwa sheria na twaambiwa kuwa uko mezani kwa Rais ukisubiriwa kusainiwa.

  • Hata hivo tunashangaa kuwa sheria hii haisainiwi kwa uharaka uleule ulofanya ikapitishwa bungeni.

  • Kulikoni?

  • Habari za mitaani zinasema kuwa wachimbaji wakubwa wa madini wamepeleka mezani kwa Rais malalamiko yao kuhusu sheria hiyo.

  • Cha ajabu ni kuwa malalamiko hayo hayakupitia kwa waziri wa wizara husika kitu kinachojenga hofu kuwa yawezekana baadhi ya vifungu vikaingizwa ama kunyofolewa katika sheria hiyo.

  • Si vizuri kuamini mambo ya mitaani lakini nashawishika kufanya hivo kwa kuwa pengine ni Tanzania pekee ambapo mambo yanayosemwa huwa kinyume :-(

  • Au hujawahi kusikia kuwa gesi ikianza kutumika umeme utashuka bei wakati unapanda kila leo? Au hujawahi kusikia kuwa uchumi unakuwa ilhali mwananchi wa kawaida anaishi kwa kiwango cha chini ya dolari moja kwa siku? Ni mawazo tu ya mimi mpigakura nilojichokea na kukata tamaa :-(

  • Kutokana na kauzoefu kaduchu tu ka yaliyotokea kwa sheria ya fedha za uchaguzi kwa vifungu ambavyo havikujadiliwa bungeni kuchomekezwa huko na Rais kusaini (mpaka Slaa alipopiga kelele), hatutashangaa matakwa ya wachimbaji kuingizwa kwenye sheria hiyo tunayoambiwa iko mezani kwa Rais.

  • Ikitokea hivo basi Rais atakuwa amewaangusha walomuweka madarakani kwa kupuuzia matakwa yao na kusikiliza ya wachimbaji wakubwa ambao wenyewe wanachokitaka ni faida huku wakituacha akina siye tuloitunza hazina hiyo bila mafao yoyote.
Mheshimiwa Rais, tupe raha kwa kusaini hiyo sheria hata kama si kwa namna ile ya fedha za uchaguzi ilivyofanyika :-(

Tuesday, June 1, 2010

Changu chatakiwa, chako je?

Wanataka nambari za kitambulisho changu, chako je?

Nimefikiwa na ugeni nyumbani. Tofauti na mgeni kukirimiwa yeye kaamua kunikirimia. Anasema anataka kitu kwangu na kisha atanitembelea usiku kunieleza jinsi ya kufanya.

Nimeamua kulisema hili kwa kuwa limenikera sana. Mgeni huyu anataka kitambulisho changu cha kupiga kura achukue nambari zake na pia kadi yangu ya chama anaitaka namba zake.

Swali ni kuwa anazitaka za nini? Huyu diwani vipi?

Je kadi zenu nazo zinatakiwa? Mbona sijaona popote kutangazwa popote kuwa vitambulisho hivo vinatakiwa?