Monday, May 31, 2010

Je Yesu alikuwa Mmatengo, Mngoni, Mndendeule..ama?


Nimepata ujumbe huu toka kwa rafiki yangu wa huko kusini (mkoa wa Ruvuma) na imenipa maswali ambayo naomba mnijuze.

"Kama una nguvu kipesa fanya aende aende na mke WA MIMI atasaidia kujiandaa. Mke WA MIMI alikuwa tayari lakini mimi sina pesa"

Katika biblia twasoma Yesu akiwambia watu kuwa, ".....hakuna atakayekwenda kwa Baba isipokuwa kwa njia YA MIMI"

Nimekuwa nikifuatilia mazungumzo na rafiki zangu wa kutoka Ruvuma a.k.a Sauzi nimegundua kuwa

a). Yangu hutamka YA MIMI
b). Wangu hutamka WA MIMI. Sina hakika kama YAKE nayo hutamkwa YA YEYE....lol


Mojawapo ya kitambulisho cha mtu ni LUGHA yake.

Swali:

Je Yesu alikuwa Mmatengo, Mmanda, Mngoni (kwa kifupi alikuwa wa kabila mojawapo la SAUZI)?

Ama biblia ya kiswahili ilitafsiriwa kwanza na watu wa makabila hayo ya SAUZI?

Wataalamu wa isimu (Matondo) na masimulizi (Mbele) naomba msaada wenyu!

Friday, May 21, 2010

Kumbukumbu: Watu na matukio muhimu kwangu!

Mnara wa wahanga wa Mv Bukoba!


Leo tarehe 21 Mei ni siku muhimu kwangu kabisa kwa kuwa:

Nikiwa najiandaa na mitihani katika major seminary moja jijini Nairobi Kenya, miaka 14 iliyopita tulipokea taarif a ya ajali kubwa ya Mv Bukoba ambayo ilikumba na kuua watu wasiojulikana idadi yao. Ndio, wasiojulikana idadi yake kwa kuwa watawala wetu japo wanajua wameshindwa kutuambia idadi kamili ambayo meli hiyo ilibeba.

Kwa bahati nzuri hakukuwa na ndugu wa karibu nami ambaye alipoteza maisha lakini kuna rafiki zangu ambao walipoteza ndugu. Ulikuwa uchungu mkubwa kiasi cha kutisha na kwa namna moja ama nyingine uliathiri matokeo ya mitihani kwa wanafunzi wengi wa Kitanzania tuliokuwa tukisoma hapo seminary. POLENI MLIOPOTEZA NDUGU ZENU.

Leo pia nakumbuka miaka 6 iliyopita nikiwa natokea Kigali Rwanda kwenye kikao cha kujadili athari za kimazingira zitakazotokana na ujenzi wa bwawa la umeme Rusumo kwenye mto Kagera nilipata msituko wa maisha! Nilikuwa nimeondoka hapa kijijini kwenda huko Rwanda nikimuacha mwenzi wangu akiwa Maswa kumwangalia Mamae aliyekuwa mgonjwa. Nikiwa Kigali nilikuwa nawasiliana naye kumjulia hali mgonjwa lakini baadaye nikaambiwa kuwa alihamishiwa Bugando Mwanza kwa matibabu zaidi baada ya hali kubadilika ghafla.

Wakati natua Dar saa 8 mchana nikampigia mwenzi wangu simu kujua hali ya mgonjwa na ndipo nilipokutana na kilio na kwa kuwa walikuwa na msituko nilichoweza kusikia ni 'MAMA AMEFARIKI!' Ikumbukwe kuwa wakati nikiwa kwenye ndege toka Kigali kuja Dar kupitia Nairobi nilikuwa najisikia hali ndivo sivo nikadhani kuwa kale kakichaa ka kuogopa ndege kalikuwa kanatamalaki. kumbe ni wakati huo Mama Christina Nkugi Mayenga Masanja alikuwa anapambana na kifo na ilipofika saa 7 mchana aliuacha mwili!

Ilibidi nitafute usafiri wa kwenda Mwanza kuwahi kushiriki taratibu za maziko yaliyofanyika Maswa tarehe 23 Mei.

Ni tukio ambalo lilibadilisha mtizamo wa maisha yangu kwa kuwa siyo kama yalivyokuwa wakati huyu mama yetu akiwa hai. RIP Mama Mayenga!

Unakumbukwa sana na mkwe wako Matara na Masaba; Kaka zako-Richard, Chris, na Edward; wifi zako-mama Jebe, Mama G; binti zako Bety, Jackline, Mihndi, Sekelwa, Vero na Fina; kijana wako Mzee Mayenga Jr; na wajukuu zako Emma, Edwin, Nyamtondo, Agnes, Chris na Nkugi, ; ndugu na jamaa wengine ambao hawakutajwa hapa.

Thursday, May 20, 2010

Je kasi yetu ndogo ya kutenda ndio mtaji wao?

Wakati wa kurejea almanusura niwe juu kama hao majamaa hapo!



Sikukuu ya pasaka mwaka huu imenikuta mjini Maswa Shinyanga ambako nilikwenda kumuona mgonjwa. Niliondoka Musoma jumamosi kubwa (siku moja kabla ya pasaka). Usafiri ulikuwa mbovu sana kwa maana ya kuwa magari yalikuwa yanasitasita kusafiri. Nilikaa saa 5 pale Lamadi kusubiri gari za kutoka Mwanza kwenda bariadi kupitia Lamadi.



Msafiri kafiri. Gari lilikuja likiwa limejaza ile mbaya ikawa ni wa kusimama. Nimepata nafasi ya kukaa wakati tumevuka Old Maswa tunakaribia kuingia Somanda iliko stendi kuuu kwa sasa.



Njiani ninaona vibweka kadha lakini leo nataka nizungumzie moja la muda. Ndugu zangu wasukuma wa Shinyanga na Mwanza hawana haraka. Konda anaweza kuita watu wa Sapiwi wajiandae wakati mnaondoka Mkula kwa kuwa gari limeshona ile mbaya lakini wapi. Linafika Sapiwi, Dutwa, Mwakibuga, Nyakabindi na Old Maswa ni yale yale. Mpaka gari lisimame ndo aliyeko nyuma aanze safari na mtu mmoja aweza kutumia dk 10 kushuka! Si amelipa nali bwana?



Nikasema labda hayo ni ya kipande hicho cha Lamadi mpaka Bariadi. Kuanza kipande cha Bariadi kwenda Maswa yakawa ni yaleyaleee! Vituo vya Lugulu, Mwamapalala, Nkololo (siyo Nkololo ya huko Old Maswa yaliko makazi ya Padre Ng’wanaFagani baada ya kuhama Old Maswa) nikakuta ni yaleyale.



Sijui kama ninaweza kusema kuwa wasukuma wote wako ‘slow’. Lakini mfano huu unatufikirisha sana tunapojadili suala la maendeleo. Na hapo kwa mfano huu, naona kama mustakabali wa maendeleo yetu unaweza kuwa unafuata ‘trend’ ya namna hii.

NO HURRY IN AFRICA ni msemo ambao baada ya kuona haya naweza kusema kuwa kwa kiasi fulani unashahibiana. Kwa mawazo yangu ni kuwa maendeleo yetu yanatatizwa na kutochukua hatua haraka.



Watani wa wasukuma wanasema kuwa msukuma ni mtu mwema na wakati mwingine mjinga sana kwa kuwa aweza kuwa kafungwa pingu lakini ukimuuliza kuna shida gani atasema ‘nduhu tabhu’ yaani HAKUNA SHIDA.



Utaona kuwa yanayotokea sasa ktk nchi yetu ni kwa kuwa tumeshindwa kuchukua hatua; tunaumia lakini tunasema HAKUNA SHIDA! Na maoni ya mwana-blog mmoja pale kwa Da Koero amesema ‘….wananchi kukaangwa na fedha zao, tuchange fedha ziwawezeshe kuingia madarakani kisha tukione cha mtema kuni’.


Tutafakari



Saturday, May 15, 2010

Mwanamke anapoingia Choo cha kiume ilhali choo hicho ni cha kusimama inakuwaje?

http://www.thegioiwallpaper.com/images/wmwallpapers/Candle-Love-Sign-1.jpeg
Baadhi yetu tumewahi kupenda na kupendwa. Lakini sina hakika kama tunaelewa manake. Hii inachanganya sana mpaka baadhi ya wenzetu wameandika kuhusu vipengele vya upendo huo. Da Yasinta kaandika hapa Ruhuwiko na pia hapa Kapuliya kisha Dada Muamshaji naye akaandika.

Lakini ni nini hiki?

Leo nitazungumzia kwa ufupi juu ya tafakuri juu ya kupenda/upendo katika mazningira ya kiafrika. Asubuhi ya leo wakati natoka bafuni kuoga nilikumbana na mtangazaji wa TBC1 katika kipindi cha Taarabu.

Bibie huyo alikuwa anasoma sms zilizotumwa kwake na moja iliyotoka kwa mkaka mmoja ilisema "...nakupenda sana". Yule mtangazaji akaitazama sana kisha akatabasamu na kusema "...nimeolewa!"

Hii imekuwa imeleta maswali mengi sana kwangu kwa nini alisema hivyo. Hii imenipa kila sababu kuamini kuwa katika mila ya kiafrika mtu akimwambia mwanaume/mwanamke 'NAKUPENDA' basi manake ni kumtaka kimapenzi.

Katika mila ya wenzetu (nimepitapita huko japo uzoefu wangu ni very limited) mwanamke/mwanaume anaweza kumwambia mbinti/mkaka "would you mind having a cup of coffee together" na akakubali na kama hana nafasi atamwambia hana nafasi mpaka wakati mwingine. Ikitokea hivo kwa mkaka/mdada wa kibongo wa kuombwa kunywa soda na mtu mgeni ambaye hawajawahi kuonana atasema 'nimeolewa/nimeoa'. Kwa nini iwe hivyo wakati hakumuuliza kama ameolewa/ameoa?

Swali: Je mtoto wa kiume/kike akimwambia mama/baba yake kuwa ampenda anamaanisha kumtaka pia kimapenzi?



Je mama/baba akimwambia mtoto wake wa kiume/kike kuwa ampenda anamaanisha kumtaka pia kimapenzi?




Je mtoto wa kiume/kike akimwambia dada/kaka yake kuwa ampenda anamaanisha kumtaka pia kimapenzi?


Kama siyo hivyo kwa majibu ya ndio kwa maswali hapo juu je ni kwa nini mtu msozaliwa naye tumbo moja akiambiwa neno nakupenda akili yake humtuma kuwa ni kutakiwa kimapenzi?

Ndiyo sababu inashangaza pale mdada anapoingia choo cha kiume na shida inakuwa pale choo hicho kinapokuwa ni cha kusimama!

Wednesday, May 12, 2010

Kurukaruka kwa Maharagwe HAIMAANISHI YAMEIVA-Mjomba!

Leo hakuna picha dunia nzima! Hivo kwa habari hii fumba macho uone picha yoyote uitakayo fikirani...lol

Leo karibia na kumalizika na kikao nilichokuwamo hapo Blue Pearl Hotel (Ubungo Plaza) aliingia mrembo binti wa kimasai aliyewahi kuwa Miss Universe Tanzania, 2008.

Alipewa nafasi ya kujitambulisha na akasema yeye ni nani na anafanya nini kwa sasa. Mojawapo ya shughuli zake ni kujihusisha na shughuli za kijamii. Alieleza juu ya kila mtu (mume ama mke) kutekeleza jukumu lake la kuutengeneza ulimwengu uwe pahala pema pa kuishi.

Baada ya maelezo yake nikakumbuka kikao tulichofanya pale Hotel Moevenpick na Blue Pearl kwa siku mbili kuhusu tasnia ya blog. Moja wapo ya mambo tuliozungumza ni kuhusu namna ya kutegemezana katika kublog. Hoja hii ilikuja hasa tulipojadiliana na kuona changamoto iliyopo ktk kublog hasa kwa Bloggers wa kike.

Ukweli ni kuw bloggers wa kike Tanzania (walio ndani na nje ya nchi) ni wachache. Na kwa kuwa siku za hivi karibuni bloggers hao wamekuwa wakishambuliwa na wanaojulikana kama ANONYs ambao kwa namna moja ama nyingine wamekuwa wakirudisha nyuma juhudi za bloggers wetu wa kike kutuletea mtizamo wao wa namna ya kuufanya ulimwengu (kwa maana ya Tanzania yetu) uwe pahala pazuri pa kuishi.

Ni kwa mantiki hiyo bloggers hao ambao walikutana kunywa chai/kahawa hapo waliweka azimio la kuwataka bloggers wa kiume kuwapa SAPOTI wenzao wa kike ili wasijekata tamaa wakaacha ku-blog.

Sasa unaweza kumtazama huyo mrembo nilokutana naye hap Amanda Alfred na hapa Amanda Alfred!

Kwenyu, Anonys, karibuni CHAI...ndo kwanza ngoma imeanza kwani kama asemavo mjomba hapo juu "Kurukaruka kwa maharage si kuiva kwake!"

Sunday, May 9, 2010

Dar Leo!

Dar leo hii kutokea Hotel moja jijini ambapo bloggers walikutana kubadilishana mawazo!


Pamoja na kubadilishana mawazo walikunywa kahawa kwa raha zao!

Friday, May 7, 2010

Wikiendi Njema



Napenda kuwatakia mwisho wa wiki mwema kwa kaujumbe hako hapo chuu huku mkitafakari kuianza wiki ichayo vema!

Wednesday, May 5, 2010

Kumbukumbu: Miaka 2 bila Munga Tehenani

Leo imetimia miaka miwili tangu mtaalam na mwalimu wa Utambuzi Munga Tehenan afariki. Alifariki tarehe 5 Mei 2008 na kuzikwa pale makaburi ya Kisutu. Siku chache kabla ya kufariki aliandika makala isemayo 'HII NI MAITI YA NANI?'. Hii ilikuwa kama utabiri wa kitakachotokea na kwa waliokuwepo msibani wanaelewa kuwa kulitokea kama makala ilivyoeleza.

Tangu afariki na Gazeti la Jitambue kutokuwa hewani/mitaani kumekuwepo/kumejitokeza ombwe la maarifa ya utambuzi. Bila shaka wanafunzi wake wanafanya kila liwezekanalo kuwezesha gazeti hilo liwe mitaani kwani kwa hali ya sasa elimu hiyo inahitajika.

Nakukumbusha makala hiyo kwa kuisoma hapa chini. Na ukitaka kusoma makala za Utambuzi ambazo baadhi ziliandikwa katika gazeti la Utambuzi waweza kusoma katika Utambuzi na Kujitambua; na waweza kujikumbusha mengine hapa:

========

HII NI MAITI YA NANI!!!!!

Nilipokuwa mwanafunzi wa sekondari, niliwahi kushuhudia mwili wa mwanafunzi mwenzetu ukigombewa na wazazi wake. Huyu mwanafunzi mwenzetu alifariki ghafla shuleni na ikabidi wazazi wake wafahamishwe ili waseme maiti isafirishwe kwenda wapi.

Mama alisema, maiti ya mwanaye ibaki hapo alipofia, kwani atakuja kuichukua na kuisafirisha kuipeleka kwao (mama) kwa mazishi. Baba naye alisema hivyo hivyo. Walimu wakaamini kwamba, baba na mama wanazungumza jambo lilelile. Lakini walipowasili pale shuleni, ndipo walipogundua kwamba, hawakuwa wanawasiliana na watu walio pamoja.

Baba alikuwa na dini nyingine na mama alikuwa wa dini nyingine na walishaachana kitambo. Tangu walipoachana wazazi hawa, kila mmoja akawa anamvutia mtoto aingie au afuate dini yake. Kwa jinsi tulivyokuwa tunamfahamu marehemu, hakuwa hasa mtu wa dini fulani. Wakati wa vipindi vya dini, huyu mwenzetu alikuwa anaingia mara kwenye madarasa ya waislamu, mara wakristo na alikuwa anaingia kwenye madhehebu mbalimbali.

Basi, wazazi hawa walikuwa kila mmoja akitaka kuchukua mwili wa marehemu. Kila mmoja alikuwa akitoa maelezo ni kwa nini yeye ndiye anayestahili kumzika mtoto kwa dini yake. Malumbano haya yalikuwa makubwa mpaka vyombo vya dola vikahusishwa. Nakumbuka alikuja afisa mmoja wa upelelezi kwenye malumbano hayo. Katika kujaribu kutafuta muafaka, afisa huyu alizungumza kama vile kwa kuhutubia akisema: " Inasikitisha kwamba, kijana wetu mpendwa, anaingizwa kwenye choyo na ubabe wa kuoneshana nani zaidi, katika hali hii ambapo hawezi kujitetea. Naamini, huyu marehemu kwa sasa anawachukia wazazi wake wote, kwani anajua wazi hakuna anayempenda hata mmoja, bali wanatumia kifo chake kama uwanja tu wa mapambano ya kujitosha kwao.

Naamini, hivi sasa marehemu angeombwa kuchagua rafiki na ndugu wa kweli, angechagua wanafunzi wenzake na walimu wa dini. Hii inatokana na ukweli kwamba, hawa hawakutaka kumpangia aabudu au kuifuata imani gani ya dini. Tunaambiwa aliingia kwa waislamu, na aliingia kwa wakristo pia, hakuzuiwa au kusemewa, alikuwa huru.

Kuwa na dini ni kuwa na uhuru. Kuwa na dini ni kuwapa wengine uhuru wa kuwa wao. Kuwa na dini siyo kutumia tatizo la mwingine kujifaharisha, kuonesha ubabe na urijali ulionao. Hiyo ni kibri ambayo kwa mtu aliyepoteza mwili kama huyu kijana wetu anaiona na kuijua vizuri, haipendi hali hii..."

Hotuba hiyo ilisaidia sana, kwani hatimaye ndugu wa upande wa mama na wale wa upande wa baba walikaa chini wakiwa na adabu mpya na kujadili. Hatimaye walikubaliana kijana azikwe kwa dini ya mama yake.

Miaka 30 baadaye, nakutana tena na watu wanaogombea maiti, watu wanaoamini kwamba mzoga wa binadamu una maana yoyote. Sijawahi kuona mtu akitoa shati au gauni kwenye mfuko wa nailoni na kuvaa mfuko huo badala ya kuvaa shati au gauni, nimesema sijawahi kuona, huko ni kujidanganya. Nimekuwa nikiona sana jambo hilo, ambapo ni pale watu wanapogombea mwili.

Inaonesha wazi kwamba, binadamu bado ni mjinga sana juu ya maisha yake. Mwili, mwili ni nini, na hadi wapi? Kama mwili ungekuwa na maana sana, baada ya mtu kufariki usingekimbizwa mochuari, usingepakwa asali au usingechomwa sindano ili usiharibike na kuleta usumbufu wa harufu na maradhi. Mwili siyo mimi wala wewe. Mwili haujawahi kuwa mwenye mwili na hautakuja kuwa. Mwili ni kama tochi tu, ambayo umeiazima ili iweze kukusaidia kufika kijiji cha pili, kutokana na giza na njia ya uchochoro ambayo unatakiwa kuipita ili kufika kijiji hicho cha pili. Mwili ni kifaa na siyo wewe, bali wewe unakitumia kifaa hicho Binadamu anajibainisha kwenye maisha haya ya hapa duniani kupitia mwili wake, lakini yeye siyo mwili.

Mwili ni ubainisho, ni chombo cha kutumika kwa kusudi la kidunia tu. Baada ya muda mwili hukoma kuwepo, hujimaliza wenyewe au kumalizwa, ili binadamu amudu kuingia hatua nyingine ya maisha ambayo haitumii au haihitaji mwili. Tangu ulipozaliwa umeoneshwa na kufundishwa kwamba, wewe ni mwili kwa njia zote. Akili yako imeshika kutu kwa kuamini kwamba, mwili ni wewe na wewe ni mwili. Huna uwezo tena wa kuuona ukweli, kwa sababu vipimo vyako vyote kuhusu maisha vinaishia kwenye akili, ambayo nayo pia haikuhusu, siyo yako, umepachikwa tu.

Kwa ujinga huu wa kutojua mwili ni nini na sisi ni nani, ndipo ambapo tunaingia kwenye ujinga wa kuendeshwa na miili yetu, hisia zetu na akili. Kila mmoja anaamini kwamba, mwili wake ukipotea, ukishindwa kutumika, yaani akifa, basi huo ndiyo mwisho wake. Kama hiyo ni kweli, ina maana binadamu hana maana kabisa, ni upuuzi usiofaa kuelezewa!

Yaani binadamu amekuwepo ili awepo kwa mwezi mmoja, miaka kumi, hamsini, sabini, tisini, au mia tu. Halafu baada ya hapo basi. Huu ni uongo mkubwa sana, unaoweza kukubaliwa na akili makapi ya kulishwa tu! Anayetafakari zaidi kidogo, atabaini kwamba, mwili ni mwili tu, ni kasha tu.

Ni kasha ambalo muda wake wa kutumika ukiisha mtumiaji au [wewe] analiacha kwa sababu haliwezi kukidhi kile anachokihitaji hapa duniani. Mtumiaji anachukua kingine ambacho kinakidhi wakati huo [baada ya kifo]. Kwa hiyo, binadamu hafi bali mwili ndiyo unaofikia ukomo wa muda wake wa matumizi kwa sababu mbalimbali. Anapokufa John au Hamisi, haina tofauti. Anapokufa mkulima hohehahe au tajiri kuliko wote duniani, pia haina tofauti. Wote wanapita kwenye hatua muhimu ya mabadiliko, ambapo wanaacha matumizi ya kifaa kilicho kuwa ndicho pekee kinachoweza kuwabainisha na wengine hapa duniani na kuchukua kingine ambacho hakiwezi kuwabainisha tena na wale wenye miili bado.

Anapokufa John au Hamisi, haijalishi kama amezikwa kwa jeneza la dhahabu na mizinga 100 au kwa masululu butu na kaniki. Kuzikwa ni utaratibu wa kimazoea wa kuhifadhi mwili ambao sasa ni mzoga tu, ili usisumbue watu wengine kwa harufu na maradhi. Kuzika haina maana kwamba, kunambadili aliyekuwa akitumia mwili huo [marehemu], la hasha. Kama unadhani kwamba Mungu anahesabu umezikwa na dini gani, umezikwa na shehe au padri gani, ndiyo afanye uamuzi wa kukupokea mbinguni au hapana, ujue unahitaji msaada wa haraka, kama siyo kupelekwa milembe. Ujue hujui chochote ingawa umekuwa ukujidanganya kwamba unajua.

Mungu wa kweli hahangaiki na mzoga, bali sisi kwa ufinyu wetu ndiyo tunaodhani kwamba, mizoga au[maiti] hii ina maana. Mara nyingi nimekuwa nikiwaambia jamaa zangu, ‘nikifa, mtaangalia ni mazingira gani ni rahisi kwenu kuutupa au kuuhifadhi mwili wangu. Kwa nini? Kwa sababu, kama sikuwa karibu na Mungu wakati nikiwa na mwili, huo, ukaribu utaletwa leo wakati nimeupoteza mwili huo kwa sababu tu, mwili wangu umezikwa kwa dini ya babu yangu? Ukosefu wa ufahamu wa kiwango kikubwa sana. Kama nilikuwa karibu na Mungu wakati wa uhai wangu, basi hata nikitupwa ****** baada ya kufa, ukaribu huo hautakufa. Mungu hayatazami mambo kama Abdallah Juma au John Maiko! Kwani kuzika hasa ni kitu gani?

Hatuziki watu ili waende mbinguni. Kama ni hivyo, wanaoliwa na wanyama, kuungua na kuteketea kabisa, wao Mbinguni hawatafika? Kama hawatafika, watahukumiwa vipi siku ya mwisho? Mwili hautakiwi Mbinguni, hauna kazi huko, kwani huko siyo makazi ya miili. Mwili unafaa tu duniani Kuna zile jamii ambapo mtu akifa mwili wake huchomwa moto na kuteketezwa kabisa Unadhani hizi jamii hazimjui Mungu kama wewe unavyomjua? Zinamjua, tena pengine vizuri zaidi yako. Lakini, zimeng’amua kwamba, mwili ni kasha tu, likishindwa kufanya kazi, ni sawa na taka nyingine, hutupwa dampo na kuteketezwa kwa moto. Mtu akishauacha mwili wake [kufa] hana tena uhusiano na mwili huo. Mtu huyo anakuwa ameingia kwenye awamu nyingine ya maisha ambayo haihitaji mwili na ambayo haihitaji kujua huo mwili umezikwa na nani na wapi. Ni akili isiosogea ndiyo ambayo inashindwa kufanya mikokotoo midogo kama hii.

Ukiona watu wanagombea maiti, jua kwamba, hata kama wamevaa masuti na kubandika digrii zao kwenye kila ukuta, ni watoto wadogo kiufahamu. Ukiona mtu pia anaacha wosia mrefu wa namna anavyotaka akifa azikwe, naye huyo ni mpujufu tu wa ufahamu. Kwa nini? Unagombea kuuzika mwili wa fulani ili upate kitu gani, ili huyo marehemu naye apate nini? Hata usipouzika, kumbuka kwamba, ameshakufa na ukiuzika, ameshakufa pia. Haifanyi tofauti yoyote kwa kweli. Kama nilivyosema awali, huuziki mwili ili uende Mbinguni kwa sababu mbingu haiko ardhini. Unaufukia ili usisumbue kwa harufu.

Ukienda kwenye nchi zenye vita hasa vya wenyewe kwa wenyewe, utagundua kirahisi kwamba, maiti hana maana, maiti ni msumbufu kwa kunuka na kusambaza magonjwa. Tunazika kwa sababu tuna nafasi ya kuhifadhi mwili kwa heshima na taratibu ambazo zinaonesha kujali mwili wa mwenzetu ambao ulitumika kufanya mema au maovu. Kwenye kizuizi na misukosuko au vita, hakuna anayeweza kukumbuka, siyo kuzika bali hata kufukia maiti. Kila mmoja anafikiria kuendelea kubaki na mwili wake kwanza. Aliyepoteza wake, basi hakuna anayemjali, kwani haina maana kabisa kumjali. Hata aina nyingine za mazishi zinaonesha tu ujinga na utoto wa binadamu.

Mazishi ya kifahari yenye kuhusisha majeneza ya dhahabu na vyakula na vinywaji vya bei mbaya. Ni ujinga uliopindukia kwa sababu, inawezekana kabisa marehemu au wanaotoa fedha hizo hawajawahi kumsaidia aliye hai hata kwa chupi ya mguu. Sasa kusaidia huo mzoga kwa mapambo inaongeza kitu gani? Nimesema unapoona mtu anaacha wosia ili azikwe vipi, wosia ambao wakati mwingine ni kero tupu, ujue huyo naye ni mtoto wa miaka sita, bila kujali anamiliki au amesoma hadi kiwago gani. Ni utoto kwa sababu, unapoacha mwili, siyo kazi yako kusema huo mwili ufanyiwe kitu gani. Waliobaki, wanaweza kuamua kuuchoma mishikaki [kama wanakula watu], wanaweza kuukausha na kuuweka kwa maonesho, wanaweza kuufukia kwenye kijishimo cha futi tano na ukafukuliwa na fisi usiku, na wanaweza kuuzika kwa matarumbeta na sanduku la dhahamu. Ni hiari yao. Ukishauacha mwili huna mamlaka nao tena.

Ni wale waliobaki ndiyo wanaolimbuka nao tu. Nimekuwa nikitazama hii tabia ya kugombea maiti kwa jicho lenye mashaka na ufahamu wa binadamu, hofu zake na ufisadi wa nafsi alionao. Mtu amekufa, wewe unasema nataka nimzike mimi, sawa. Kwani mbona huendi hospitalini ukaulizia maiti ambazo hazina ndugu na kuzichukua ili ukazizike? Wewe si unapenda kuzika na unaamini kumzika mtu kwa dini yako ni jambo kubwa na la maana sana? Pia hospitalini, utapewa maiti nyingi zisizo na ndugu. Ukishazipata zibadili majina na kuziingiza kwenye dini yako kwa mujibu wa utaratibu wa dini yako. Halafu zika! Hiyo huitaki kwa sababu haina maslahi, haina kuonesha ubabe ambao umefundishwa na wazazi, na jamii na pengine hata na dini yako hiyohiyo. Kugombea maiti ni kujiogopa.

Kugombea maiti ni kujitafuta kimakosa. Kugombea maiti ni kutojua dini. Kugombea maiti ni kudhani mtu anaweza kuwa na uhuru wa kuwa mtu mwingine. Kugombea maiti ni kufikiri wewe ni mwili, Kugombea maiti ni njaa ya mali au haja ya kupanda kithamani. Kwa ujumla ni ubabe wa kimtaa zaidi. Mara nyingi imeshatokea, anapookotwa maiti na watu wakaanza kuulizana, jamani maiti hii ni ya nani? Ujue maiti hiyo itazikwa na serikali. Hakuna mtu au kundi la kidini la eneo hilo ambalo litajitokeza kuichukua na kuizika maiti hiyo kwa imani yake. Hilo haliwezekani kwa sababu halina utamu.

Halina kubishana, halina kulumbana, halina ujuaji na ubabe. Anasubiriwa mtoto mwenye mzazi walioachana na walio na dini tofauti. Huyu akifa, hasira na visasi vyote vya nyuma vinaishia kwenye mwili wake. Atasubiliwa yule ambaye alishakuwa kwenye dini yetu akatoka, huyo akifa
tuna sababu ya kugombea maiti. Kama nilivyosema, hapo kuna malumbano na ujuaji na kuoneshana. Halafu bado mnajiita mnatumikia dini, zipi? Ni ujinga tu.

Monday, May 3, 2010

Aisifuye mvua IMEMNYEA!



Kwa watu wa Dar na maeneo ya Pwani kwenye joto jingi huwa wanapenda mvua ili walau ipunguze JOTO.Kwa watu wa vijijini kama siye hupenda mvua ili ituwezeshe kulima !

Lakini mvua ya mwaka huu inachanganya sana. Kwangu mimi (kama watu wa Dar wanavolalamika) imeanza kuonesha athari kubwa sana.

Bustani yangu inaanza kufa kwa kuwa kumejitokeza chechemi ambayo inafanya miti yote kuanza kufa.

Washauri wa kienyeji wananishauri nipande mkaratusi lakini huo ni mojawapo ya miti ninayoichukia kabisa kutokana na untumiaji wa maji kwa wingi hasa ikikua. Kwa wastani naambiwa mti mkubwa wa mkaratusi unalamba lita 1000 kwa siku. Sasa mie nnayetaka kutumia kasehemu hako ninakoishi kwa ajili ya mbogamboga na matunda si ntaula wa chuya?
Sasa mvua imeleta kidamisi kotekote!

Msaada toka kwa wataalamu, hii chemchemi vipi?