Tuesday, February 23, 2010

Je twamaanisha tukisemacho kweli?





Shule zetu na maandalizi ya kizazi kipya!!!
Taifa la kesho?









Kila siku tumekuwa tukisikia juu ya serikali yetu kutilia mkazo juu ya elimu ya msingi na kadhalika. Hata hivyo sina hakika kama hili lina kuwa na maana kwa kuwa ukiliangalia kwa undani utaona kuwa ni kama tunacheza mchezo wa kuigiza!

Kwa mujibu wa waraka wa elimu (sijui niiite sera) wa 1995 serikali yetu iliazimia kuhakikisha kuwa elimu ya awali inatiliwa mkazo katika kila jambo.

Leo hii timu yetu ya mpira ikifungwa ama Yanga na Simba zikishindwa utasikia wakubwa wanasema 'kuna haja ya kuhakikisha kuwa vipaji vinaibuliwa kuanzia utotoni'!

Picha hii hapo kulia ni shule ya awali a.k.a chekechea ambayo niliikuta kijiji cha Loswaki kilichoko kata ya Terat wilaya ya Simanjiro nkiwa huko kishughuli. Hii ni shule inayotegemewa kuibua vipaji na kutoa viongozi na wataalam wa kizazi kijacho!

Nasema hivo kwa kuwa kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Asasi ya MWDA ya Mwanza huko wilayani Kwimba ulionesha kuwa wakati shule za msingi kuanzia madarasa ya kwanza mpaka saba wanapewa ruzuku, aidha hakuna madarasa ya awali (kama inavoelekezwa ktk sera) ama kama yapo hayapewi ruzuku kama inavotakiwa kwa mujibu wa sera zilizopo.

Cha kushangaza ni kuwa viongozi wetu ni kama hawaelewi kitu wanachokiweka ktk makaratasi iwe ni ktk sera ama sheria zinazotungwa pale mjengoni au hawataki kuelewa kwa makusudi.
Kama ni kwa makusudi tuna haja ya kuwa na watu kama hawa ambao wengine wakiwa ni wataalamu waliobobea katika taaluma zao?

Je tumefikia hatua ya kuamini kuwa hakuna lolote tunalolipanga ambalo litakamilika ati kwa kuwa walioko Tanzania (Dar) hawataki, hawaelewi ama hawawezi kuchukua hatua katika kuhakikisha kuwa elimu yetu inakuwa ya maana kama kule ambako wao hupeleka wana wao kusoma?

Je ndiyo sababu ya kuanza kudharau taaluma ya ualimu kiasi cha kuanzisha program za ualimu za ' voda fasta' ambapo vijana wetu (wenye msingi mbovu wa elimu) wanaingizwa ktk program ya kuwa walimu kwa muda wa miezi 6 tu!

Nadhani haitoishia hapo kwa kuwa sekta itakayofuata yaweza kuwa AFYA ambapo madaktari bingwa wa upasuaji wakwenda mafunzoni kwa muda mfupi! Na ikitokea hivo basi TUTAOMBA kwamba watu wa kwanza watakaofanyiwa upasuaji wawe wale wanaopata matibabu yao nje ya nchi!!!!!

TAFAKARI!

Saturday, February 20, 2010

Rushwa na kutowajibika ni laana?

Simba wa Serengeti

Jumanne wiki hii nilikuwa safarini kutoka Musoma kwenda Arusha kuzurura kijasiliamali! Ninapatwa na kigugumizi kuamini kile nilichokiona na kukisikia kuhusu mbuga ya Serengeti.

Wakati tukiwa tumevuka geti la Naabi gari ya mbele yetu ndogo ilokuwa ikisafiri kwenda Dar ilisimamishwa na kuambiwa iwekwe pembeni. Sisi tulokuwa katika mwendo kama wa marathoni tuliona jamaa alokuwa amejificha nyuma ya gari lenye nembo ya SENAPA na namba SU akitumulika kwa kifaa chenye rangi ya krimu cha kupimia mwendo kasi kisha akaweka mkono kama wafanyavyo askari wa usalama barabarani.

Jamaa akatwambia kuwa tupunguze mwendo na tukaruhusiwa kuondoka huku tukiwa na maswali lukuki kuwa ni kwa nini wenzetu wamebaki.

Tulikutana nao Karatu na wakatwambia kuwa wamelipishwa faini ya sh 20,000/= na hawakupewa risiti kabisa. Wakasema kuwa jamaa alokuwa amevaa t-shirt ya rangi nyekundu aliwang'angania kuwa warejee Naabi wakalipe faini ya sh. 50,000/= ili waendelee na safari. Jamaa kwa kuwa walikuwa wansafiri kwenda Dar wakasema hawatarudi huko takribani km 20 (jirani tu na mpaka wa Serengeti na Ngorongoro) kwa kuwa hao jamaa walipaswa kuwa na vitabu vya faini ili wawalipishe hapo na kuondoka zao. Haikuwezekana. Jamaa na dereva wake akadai kuwa wakatiwe 20,000 waruhusiwe kuondoka.

Kuna maswali kadhaa hapa:
  • Je huu ni mradi wa wakubwa au wa hawa wadogo wanaojaribu kuitia dosari idara hii ambayo imekuwa na malalamiko zaidi?
  • Wakubwa najua kuwa haya yanatokea au wanakaa tu ofisini na kuacha mambo yaende kama yalivo?
  • Je ni halali kuwalipisha watubila risiti ni wa SENAPA tu ama wa mbuga zote?
Wakati narejea Musoma nimeongea na baadhi ya madereva na wakaniambia kuwa faini zinaanzia 10,000 mpaka 100,000 kulingana na kosa na unatozwa papo kwa papo na kupewa risiti. Sasa hiki kituko cha wapi?

Kama wanaopaswa kuhakikisha hali ya usalama wa wanyama wako namna hii, vipi pale kwenye makusanyo ya mapato mengine? Je si kuna uwezekano kuwa hayo mapato tuambiwayo yanapatikana ktk sekta ya utalii si halisi?

Je rushwa ya namna hii inayoonekana katika kila sekta sasa, ni laana?

TAFAKARI

Monday, February 15, 2010

Ni Kweli Tunazinduka ama Tunazinguka?


Rais JK akizindua kampeni ya 'Malaria no More' Jijini Dar Juzi


- Rais wa Tanzania Ndugu Jakaya Kikwete amezindua kampeni ya Zinduka jijini Dar. Amesema sisi tuwe kizazi cha mwisho kufa kwa malaria. Hali halisi ikoje?

- Wakati Dr Magufuli anaendesha zoezi la kutafuta wavuvi haramu huko bwawa la nyumba ya Mungu alikuta kuwa zaidi ya asilimia 70 ya nyavu zilitokana na vyandarua vile vinavyotolewa kwa akina mama wajawazito :-(

- Wakati zoezi la kugawa vyandarua Tanzania lilpokuwa linafanyika mwaka jana,walipokuwa wilayani Bunda, wagawaji walishuhudia mama mmoja akitumia chandarua alichogawiwa kwa ajili ya kutumika kama kivuli (shade) ya bata na kuku wake :-(

- Wiki mbili zilizopita nilipokuwa kijiji cha Marasibora kilichoko kandoni mwa mto Mara, nilishuhudia vyandarua vikitumika kujengea vivuli vya kuku na mabata :-(

- Nilishikwa na butwaa zaidi kuona kwamba hayo yanafanyika katika sehemu usizotegemea kwani nilishuhudia vyandarua lukuki (vyeupe/blue) vikiwa vimetundikwa kama vivuli vya mabanda ya kuku na bata nyumbani kwa aliyewahi kuwa Katibu Mkuu Kiongozi enzi za Mwalimu, Mzee timothy Apiyo :-(

Si ajabu ukakuta jamii za pembezoni mwa Ziwa Nyanza (Victoria) vyandarua vinavogawiwa kwa wanajamii wa huko huishia kuvulia dagaa :-(

Swali ni: je kwa nini hali inakuwa hivi?

TAFAKARI!

Thursday, February 11, 2010

Dhahabu ama Watu wetu?














Mwaka jana katika mwezi wa Mei kulitokea kuvuja kwa maji yenye kemikali ambazo zilihofiwa kuwa za sumu ambazo zilisababisha madhara makubwa kwa binadamu na wanyama katika mgodi wa dhahabu wa North Mara huko Tarime.Bofya hapa katika kurasa hizi uone kimbembe hiki North Mara,Tighite River,North Mara, North Mara, Mkanganyiko Bungeni.

Madhara ya uharibifu huo ni makubwa kwa mujibu wa viongozi wa vijiji vinavyozunguka mgodi huo Kibasuka.

Ona picha hizo :-(
Hawa walitumia maji ya mto Tighite wakaishia kuwa hivyo :-(

Wakati akitoa maoni yake mbunge mmoja (Job Ndugai) alisema 'tukipewa kuchagua kati ya dhahabu ama watu wetu, basi nina hakika tutachagua watu wetu'.

Cha kushangaza ni kuwa kuchukuwa hatua kwa swala hili kumekuwa kukichukua muda mrefu sana. Tunachosikia ni majibu ambayo ni ya kiutawala ambayo Barrick, DC wa Tarime, RC Mara, NEMC, Wizara ya Mazingira, Wizara ya Afya na Wizara ya Madini wanayatoa ni sawa kuwa 'wenyeji wameiba lining za mabwawa ya kuhifadhia maji machafu'. Je na hawa ambao wako katika vijiji vilivyo mbali na mgodi ambao ndo wamedhurika kwa kiasi kikubwa ni wezi?

Ndo kusema kuwa wataalamu wetu wa afya kuanzia Mkemia Mkuu wamewaasi wananchi walowasomesha kwa jasho la kodi zao na kuungana na wawekezaji kwa kisingizio cha 'attracting foreign direct investment? FDI kwa gharama za wananchi wetu? Je kuna mkono wa mtu (kisiasa na kampuni)ama ni kutojali kwa viongozi wetu?

TAFAKARI!

Karibuni Kijijini Kwetu

Napenda kuwakaribisha katika kijiji cha stori! Msukumo huu umetokana na ninyi wadau kunitaka nijiunge nanyi. Sina hakika kama nitaweza kuvaa viatu vyenyu lakini TUPO PAMOJA!